Habari

Viongozi wataka kaunti itenge pesa za kununua bunduki na risasi

Na DAVID MUCHUI April 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

VIONGOZI wa Meru wanataka serikali ya kaunti itenge fedha za kununua bunduki na risasi ili kuimarisha vita dhidi ya wezi wa mifugo katika sehemu za kaskazini mwa kaunti hiyo, hatua ambayo huenda ikapingwa na serikali ya kitaifa.

Viongozi hao walizungumza Jumamosi wakati wa mazishi ya polisi watatu wa akiba waliouawa Aprili 7, 2025, wakisema wizi wa mifugo katika Igembe Kaskazini umefikia kiwango cha kutisha na unahitaji juhudi za pamoja kuukomesha.

Walipendekeza hatua zichukuliwe na serikali ya kitaifa pamoja na ile ya kaunti kukomesha uhalifu huo.

Moses Mungathia, Robert Mwenda na Martin Kinyua waliuawa kwa kupigwa risasi Aprili 7 baada ya makabiliano makali ya risasi kati ya polisi na wezi wa mifugo.

Bunduki zao tatu ziliibwa lakini zilipatikana wiki iliyopita. Mazishi yalifanyika siku ambayo polisi wa Laare walipata zaidi ya mbuzi 70 waliokuwa wameibwa.

Wakiongozwa na Gavana wa Meru Isaac Mutuma, Seneta Kathuri Murungi, Wabunge Julius Taitumu na Dan Kiili, viongozi hao walilaumu serikali kwa kutoa maneno matupu kuhusu masuala ya usalama.

Bw Murungi alitaka fedha za kaunti zitumike kutatua tatizo la wizi wa mifugo.

“Serikali ya kaunti inapaswa kutumia fedha zake kulinda wananchi. Fedha zitengwe kununua silaha na kupeleka walinzi wa kaunti katika maeneo yaliyoathirika,” Seneta alisema.

Seneta huyo, ambaye anatambua kuwa hatua hiyo itapingwa na serikali ya kitaifa, alisema ataitetea serikali ya kaunti katika Seneti kwa kutenga fedha za kununua silaha ili kupambana na uhalifu huo.

“Ninajua usalama ni jukumu la serikali ya kitaifa lakini fedha za kaunti lazima zitumike kulinda watu. Nawasihi MCAs watenge fedha kwenye bajeti ijayo,” alisema.

Kauli yake inajiri wiki moja baada ya Gavana Mutuma kumwomba Rais Ruto kuwaruhusu wakazi wa Meru kujihami dhidi ya wezi wa mifugo.

Hata hivyo, Rais Ruto, ambaye alikuwa kwenye ibada ya Kanisa la African Independent Pentecostal Church, alimwambia gavana kuwa serikali yake itakomesha uhalifu huo.

“Gavana, hakuna haja ya kuwapa watu silaha kwa sababu tutakomesha wizi wa mifugo kama tulivyofanya Kaskazini mwa Bonde la Ufa,” Rais Ruto alisema.