Habari

Viongozi wataka mitandao ya ngono ifungwe

June 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MISHI GONGO

VIONGOZI wa kidini wameiomba serikali kufunga mitandao ya kuonyesha filamu za ngono nchini ili kudhibiti mimba za mapema miongoni mwa vijana.

Walisema haya baada ya nchi kuripoti kuongezeka maradufu kwa mimba za mapema tangu kuzuka kwa janga la corona.

Viongozi hao walilaumu mitandao ya filamu za ngono, nyimbo za matusi na kuzembea kwa wazazi katika majukumu yao kuchangia katika mimba za mapema.

Akizungumza na Taifa Leo hapo Jumatano, Mwenyekiti wa kitaifa wa Baraza la Kitaifa la Ushauri kwa Waislamu (KEMNAC) Sheikh Juma Ngao, aliwalaumu wazazi kwa kukosa kuwapa watoto wao maadili mema.

Sheikh Ngao alisema wazazi wengi wanajitahidi kuwapatia watoto wao bidhaa mbalimbali na kusahau kuwapa nasaha za maadili mema.

“Wazazi wamewanunulia simu watoto wao, wamewawekea vifurushi vya data lakini hawafuatilii wanayofanya katika simu hizo,” akasema.

Alisema kupitia simu hizo, vijana wanaangalia filamu za ngono kisha kushawishika kujaribu waliyoyaona katika filamu hizo.

Alisema kuna haja ya serikali kuanzisha elimu itakayowalenga wazazi ili kuwafunza namna ya kuwapa watoto wao malezi bora.

Aidha, aliwanyooshea kidole cha lawama wanamuziki wanaotunga nyimbo zilizo na maudhui ya ngono.

Alisema maudhui muhimu katika jamii ni kilimo, kukemea ufisadi, kutunza mazingira na maudhui mengine ya manufaa.

“Baada ya kubalehe vijana huwa na matamanio ya kujiingiza katika ngono, muziki na filamu wanazoziona zinawasukuma katika kujiingiza katika kufanya ngono kiholela. Matokeo ya hali hiyo ni mimba za mapema na kuambukizwa virusi vya Ukimwi,” akaeleza.

Aidha aliomba serikali kuweka mikakati ili kudhibiti mkurupuko wa vilabu vya pombe katikati ya miji ya watu.

“Sehemu kama Mtwapa na Bamburi vilabu vya pombe vimesheheni katika miji ya watu hivyo kufanya rahisi kwa watoto kupata vileo na wakiwa katika hali ya ulevi ni rahisi kwao kujitosa kwa ngono za kiholela,” akasema.

Katibu katika baraza la Maimamu na wahubiri nchini Sheikh Mohammed Khalifa alisema kuwa ni muhimu kwa wazazi kukumbatia majukumu yao ili kudhibiti watoto wasije wakaangamia kimaadili.

Aliwasisistizia wazazi kuepuka kuwapa wasaidizi wao wa kazi za nyumbani jukumu la kuwalea watoto.

Aidha aliwaomba wazazi kuzuia watoto kuhudhuria shughuli za usiku kujivinjari na kujitosa kwa anasa zisizofaa.