Vita ODM vyafufua mizimu ya 2022
MVUTANO ndani ya chama cha ODM umechukua mkondo mpya baada ya Katibu Mkuu, Edwin Sifuna kufufua upya masuala tata yaliyoandama Uchaguzi Mkuu wa 2022, akimlaumu Mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohamed kwa madai ya ubadhirifu wa fedha na uzembe.
Kauli za Sifuna, zilizotolewa Januari 3, 2026 katika mazishi ya Alice Wangari Gakuya huko Murang’a, zimezua mjadala mpana ndani ya upinzani na kufungua majeraha ya kisiasa kwa wale ambao hawakupona kufuatia kushindwa kwa Raila Odinga kwa tofauti ndogo ya kura katika uchaguzi uliopita.
Akizungumza mbele ya viongozi wakuu wa upinzani akiwemo aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Sifuna alimlaumu Junet kwa kulaumu hadharani mchango wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, akisema ni fedheha kumlenga kiongozi aliyebeba mzigo mkubwa wa kampeni ya Azimio, hususan Mlima Kenya.
“Kwa mara ya kwanza Baba Raila Odinga alipata kura zaidi ya milioni moja Mlima Kenya. Hiyo haikuwa bahati, ni kwa sababu Uhuru Kenyatta alitusaidia kwa hali na mali,” Sifuna alisema, kabla ya kudai kuwa baadhi ya viongozi walitumia visivyo fedha hizo badala ya kuzitumia kulipa maajenti wa chama.
Akielekeza lawama moja kwa moja kwa Junet, Sifuna alihoji ni lini fedha za Uhuru zilianza kuonekana kuwa ‘mbaya’, akimlaumu mbunge huyo kwa kutumia vibaya rasilmali za kampeni na kushindwa kulinda kura siku ya uchaguzi.
Kauli hizo zimeungwa mkono kwa njia isiyo ya moja kwa moja na aliyekuwa mgombea mwenza wa Raila Odinga, Bi Martha Karua, ambaye alisema kuwa karibu majukumu yote ya uratibu wa kampeni, ikiwemo maajenti wa chama, yalikuwa mikononi mwa Junet.
Akizungumza katika mahojiano ya televisheni ya NTV Januari 8, 2026, Karua alisema alimhimiza Sifuna “aseme kwa sauti zaidi” ili ukweli ujulikane.
“Baba alimwamini Junet kwa karibu kila kitu. Kama kuna mtu ana taarifa zaidi, aseme. Wamwage mtama,” Karua alisema, akifichua kuwa wagombea wengi walilalamika kuhusu majina ya maajenti kubadilishwa au kutokuwepo kabisa.
Karua alikiri kuwa hakuwa na uwezo wa kufuatilia kila jambo kwani alijiunga na kampeni miezi miwili na nusu kabla ya uchaguzi na alikuwa akizunguka maeneo mengi, hususan Mlima Kenya, huku pia akihitajika kwa kampeni za kitaifa.
Madai haya yanajiri wakati ambapo ODM inapambana na mgawanyiko wa ndani kuhusu msimamo wa chama kuelekea 2027, hasa baada ya Sifuna kusisitiza kuwa Raila Odinga hakuwahi kuagiza chama kumuunga mkono Rais William Ruto.
“Sisi kama ODM, Baba hakuwahi kutuambia tumuunge mkono Ruto 2027. Aliniambia Kasongo 2027 nyumbani,” Sifuna alitangaza, kauli iliyopokewa kwa shangwe na baadhi ya wafuasi na wasiwasi kwa wengine.
Hali hiyo imezidi kuchochewa na kauli ya Katibu Mkuu wa Jubilee, Jeremiah Kioni, ambaye alimshutumu Junet kwa kile alichokitaja kama kusaliti muungano wa Azimio baada ya uchaguzi.
Kioni alidai Junet alishindwa kushiriki maandamano ya kutaka Azimio itambuliwe kama muungano wa wengi Bungeni na badala yake akashirikiana na Spika Moses Wetang’ula kuzima juhudi hizo.
“Junet alifanya kazi na Wetang’ula kuzuia Azimio kupata haki yake. Leo yeye ndiye Kiongozi wa Wachache akizungumza kwa niaba ya wengi,” Kioni alisema.
Kwa upande wake, Sifuna amejaribu kujinasua dhidi ya madai ya kushambulia Uhuru Kenyatta kwa kumuomba msamaha hadharani katika mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Lugari Cyrus Jirongo, akisema baadhi ya viongozi wa ODM wamekuwa wasaliti wa kiongozi aliyewasaidia pakubwa 2022.
Wachambuzi wa siasa wanasema mvutano huu unafufua masuala ambayo yalikumba Azimio 2022 na pia ni dalili za mapema za hali ya siasa kuelekea 2027.
Kulingana na Junet Mohamed, sakata la kukosekana na kutolipwa kwa maajenti wa Azimio katika Uchaguzi Mkuu wa 2022 halikuwa kosa la uongozi wa ODM wala waratibu wa kampeni, bali lilitokana na maamuzi yaliyofanywa na watu waliokuwa karibu na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta nje ya mifumo rasmi ya chama.
Katika taarifa aliyotoa Jumamosi, Mbunge huyo wa Suna Mashariki alisema fedha zilizotengewa maajenti wa Azimio zilikabidhiwa Muhoho Kenyatta, ndugu wa rais huyo wa zamani, hatua ambayo alidai iliondoa jukumu hilo mikononi mwa chama na mgombea urais Raila Odinga.