Habari

Vita vilivyotokea katika Seneti Jumatano vinachunguzwa, asema Kang'ata

July 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MASENETA Beatrice Kwamboka na Mary Seneta wataadhibiwa kwa kupigana wakati wa uchaguzi wa uongozi wa Kamati ya Seneti kuhusu Afya mnamo Jumatano.

Inadaiwa kuwa wawili hao walichapana na kuraruliana mavazi baada ya wao kutofautiana pale Seneta wa Narok Ledama Ole Kina alipochaguliwa kuwa Naibu Mwenyekiti wa Kamati hiyo.

Tukio hilo la aibu lilisababisha uchaguzi huo kufutiliwa mbali na sasa utaratibiwa upya.

Kiranja wa Wengi Seneta Irungu Kang’ata, alisema Jumamosi kuwa uongozi wa bunge hilo umeanzisha uchunguzi kubaini kilichochochea Bi Kwamboka na Bi Seneta kupigana hadharani.

“Suala hili linachunguzwa ili ukweli kuhusu yaliyojiri ubainike. Tutachunguza kanda za kamera za CCTV na kuhoji mashahidi kabla ya kufanya uamuzi,” akasema Bw Kang’ata ambaye ni Seneta wa Murang’a.

Kiranja huyo alisema uongozi wa Seneti unachunguza nadharia mbili: kama walipigana au ikiwa walirushiana cheche za maneno tu.

Hata hivyo inadaiwa kuwa wakati wa makabiliano hayo maseneta hao wawili maalum walikabana koo. Lakini baada ya kutengenishwa na walinzi wa bunge, walidai kuwa vita vyao vilikuwa vya “kirafiki”.

Endapo itabainika kuwa maseneta hao walipigana, wataamriwa kufika mbele ya Kamati ya Nidhamu ya Seneti inayoongozwa na Spika Kenneth Lusaka.

Na endapo watapatikana na hatia wataadhibiwa kwa kuzimwa kuhudhuria vikao vinne vya Seneti.

Hiyo ina maana kuwa watapoteza marupurupu ya Sh5,000 kwa kila kikao.

Katika kikao hicho cha Kamati ya Seneti kuhusu Afya, Seneta wa Trans Nzoia Michael Mbito alichaguliwa bila kupingwa kuwa mwenyekiti.

Ole Kina pia alipaswa kuchaguliwa bila kupingwa baada ya makubaliano kuafikiwa kati ya maseneta wa Jubilee na wale wa ODM chini ya moyo wa handisheki, lakini mpango huo ukaingia mushkili.

Seneta wa Kisumu Fred Outa alimpendekeza Ole Kina kwa wadhifa huo na Bi Kwamboka akamuunga mkono.

Lakini baadaye Seneta Maalum Farhiya Ali alimpendekeza Bi Seneta kwa wadhifu huo, jambo ambalo liliwashangaza wanachama wa kamati hiyo.

Bi Farhiya sio mwanachama wa kamati hiyo lakini alikuwa amefika kumwakilisha Bi Beth Mugo ambaye hakuwepo siku hiyo.

Japo haijulikani nani aliunga mkono uteuzi wa Bi Seneta, Mwenyekiti Dkt Mbito alianzisha utararibu wa uchaguzi.

Wakati wanachama walikuwa wakijiandaa kupiga kura, Bi Farhiya aliondoka nje na kurejea akiwa na karatasi yenye sahihi ya Seneta Millicent Omanga.

“Nimeshauriana na Omanga ambaye ni mwanachama wa kamati hii kwamba nipige kura kwa niaba yake,” Bi Farhiya akasema.

Ni kauli ambayo ililakiwa na upinzani kutoka kwa wanachama.

“Hatutakubali uchaguzi huu uendeshwe namna hii,” Kwamboka ambaye ni naibu kiranja wa wachache akafoka.

“Kwa kuwa hatuwezi kuthibitisha madai ya Seneta Farhiya Ali kwamba ameagizwa kupiga kura kwa niaba ya Millicent Omanga, tutaahirisha kikao hiki,” akasema Seneta Mbito.

Baada ya uchaguzi huo kufutiliwa mbali, Kwamboka na Seneta walirushiana cheche za matusi nje ya ukumbi wa mijadala.

“Huwezi kuniambia chochote. Mimi ni mtu wa Raila Odinga na niko katika uongozi wa Seneti; nitakufunza adabu,” Kwamboka akamfokea Bi Seneta.

Kwa ghadhabu, Bi Seneta naye akamgonga Kwamboka kwa mkoba wake kabla ya Kwamboka naye kujibu kipigo kwa kumgonga kwa begi yake. Ghafla bin vu wawili hao walikamatana na kuanza kuraruliana mavazi.

Ilibidi walinzi wa bunge kuingilia kati kuwatawanya wawili hao. Baadaye Kwamboka alidai kuwa vita vyao vilikuwa vya “kirafiki”.

“Mimi na Mary Seneta ni marafiki. Hatuna uhasama wowote, lakini nitahakikisha kuwa ameandolewa kutoka kamati hiyo,” Kwamboka akawaambia wanahabari.