Vitimbi vya ‘Kamata Kamata’ vyarudi Rotich akibambwa
Na WAANDISHI WETU
IDARA ya Uchunguzi wa Uhalifu (DCI) Jumatatu ilirejelea shughuli zake za kukamata washukiwa wa ufisadi, almaarufu kama ‘Kamata Kamata’ baada ya utulivu wa miezi kadhaa.
Kufuatia amri ya Kiongozi wa Mashtaka ya Umma (DPP), Bw Noordin Haji, baadhi ya washukiwa wa sakata ya mabwawa ya Arror na Kimwarer walijisalimisha kwa DCI huku wengine wakisakwa maeneo tofauti ya nchi.
Waziri wa Fedha Henry Rotich alijisalimisha katika makao makuu ya DCI jijini Nairobi huku Afisa Mkuu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Mazingira (NEMA), Bw Geoffrey Wahungu akitiwa mbaroni katika Kaunti ya Tharaka-Nithi na kusafirishwa hadi Nairobi.
Wapelelezi pia walifika katika afisi za Mamlaka ya Ustawishaji wa Kerio Valley (KVDA) na kumkamata Kaimu Afisa Mkuu Francis Kipkech pamoja na maafisa wengine.
Lakini maswali yaliibuka miongoni mwa wananchi kama ‘Kamata Kamata’ za jana ni sehemu tu ya vitimbi ambavyo vimeshuhudiwa kufikia sasa, vinavyohusu washukiwa wa ufisadi kukamatwa ilhali kesi hazionekani zikipiga hatua mahakamani.
Kuhusiana na sakata za wizi wa mamilioni ya pesa katika Taasisi ya Huduma kwa Vijana (NYS), wengi wa washukiwa waliishia kuachiliwa huru katika sakata ya 2015.
Washukiwa 23, akiwemo aliyekuwa katibu katika wizara Peter Mangiti waliachiliwa huru na aliyefungwa ni mmoja wa maafisa aliyekuwa katibu katika kamati ya tenda, Selesio Karanja pekee kwa miaka minne jela.
Kuhusiana na sakata ya pili ya NYS mwaka jana, kesi bado zinajikokota kortini zaidi ya mwaka mmoja baadaye.
Kesi nyingine inayoenda mwendo wa kobe ni sakata ya mahindi ambapo washukiwa kadhaa walikamatwa kwenye kashfa iliyohusu kupotea kwa zaidi ya Sh5 bilioni zilizonuiwa kulipwa wakulima.