Vyama vyaamua heri ‘kuelewana’ kuelekea chaguzi ndogo Novemba
VYAMA vya kisiasa vimeamua kukumbatia mfumo wa uteuzi wa wagombeaji unaofuata njia ya maelewano vikijipanga kwa chaguzi ndogo zijazo.
Aidha, baadhi ya vyama vimelazimisha wagombeaji wao kujiondoa kusudi kupisha wagombeaji wa vyama tanzu katika miungano yao ili kuboresha nafasi ya ushindi kwa vyama vilivyoko katika Serikali Jumuishi au Upinzani.
Kwa mfano, mnamo Jumatano, chama cha Democracy for Citizens Party (DCP) chake aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua kilitangaza kujiondoa katikka kinyang’anyiro cha uchaguzi wa ubunge wa Mbeere Kaskazini ili kuunga mkono mgombeaji wa chama cha Democratic Party (DP) chake waziri wa zamani Justin Muturi.
Bw Gachagua alisema uamuzi huo ulitokana na hali kwamba Geoffrey Ruku aliyekuwa Mbunge wa eneo hilo kabla ya Rais William Ruto kumteua kujaza nafasi ya Muturi kama Waziri wa Utumishi wa Umma, alihudumu kwa tiketi ya DP.
“Tulijadiliana na kuamua kuwa ni bora DP ipewe nafasi ya kuteua mtu atakayekamilisha miaka miwili iliyosalia kama mbunge.
“Pia ni kwa msingi wa kumheshimu Bw Muturi kama kiongozi mwenye ushawishi katika eneo hilo aliye na uwezo na sifa zitakazowezesha kupatikana kwa ushindi,” Bw Gachagua akasema Jumatano, kwenye kikao na wanahabari katika makao makuu ya DCP, Nairobi.
Kadhalika, DCP ilijiondoa katika uchaguzi mdogo wa wadi ya Muumbini, Kaunti ya Makueni kuunga mkono mgombeaji wa chama cha Kalonzo Musyoka, Wiper Patriotic Front.
Pia kitamuunga mkono mgombeaji wa chama cha DAP-K kinachoongozwa na Eugene Wamalwa katika uchaguzi mdogo katika Wadi ya Kabuchai/Chwele, Kaunti ya Bungoma.
Hata hivyo, baadhi ya makubaliano yamechochea baadhi ya wawaniaji kugura vyama vyao na kujiunga na vyama vingine.
Mfano ni Diwani wa Evurore Duncan Mbui ambaye amehama DCP na kujiunga na Chama Cha Kazi (CCK) chake Waziri wa zamani Moses Kuria.
Awali, Mbui alikuwa ametunikiwa nafasi ya kupeperusha bendera ya DCP katika uchaguzi huo mdogo wa Mbeere Kaskazini.
Mwanasiasa huyo alishinda kiti cha udiwani kama mgombeaji huru katika uchaguzi mkuu wa 2022.
“Kwa kiongozi wangu mpya wa chama, Bw Kuria ninasema asante kwa kuamini ndoto na uwezo wangu na kunipa nafasi ya kuwania kwa tiketi ya chama chako.
“Kwa wafuasi wangu katika Mbeere Kaskazini, ninawashukuru kwa kuunga mkono ndoto yangu na kwa kudura za Mungu tutaibuka washindi,” Bw Mbui akasema katika mji wa Ishiara alipopokezwa cheti na Bw Kuria.
Katika eneobunge la Banissa, Kaunti ya Mandera, chama cha United Democratic Movement (UDM) kimekubali kuunga mkono mgombeaji wa chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) katika uchaguzi mdogo ujao.