Habari

Vyombo vya nyumbani vyatumiwa kupata mshukiwa na hatia ya mauaji

Na BRIAN OCHARO October 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

VYOMBO vya nyumbani vilivyoibwa viligeuka kuwa ushahidi muhimu uliowezesha serikali kuthibitisha mauaji ya mfanyabiashara wa Mtwapa, Mombasa, Jackeline Ngina Kitheka na mshtakiwa Robert Waliaula Kinisu akapatikana na hatia.

Waliuala alimuua mfanyibiashara  huyo na kuficha mwili wake ndani ya kabati katika eneo la Mtwapa miaka minne iliyopita.

Muuaji huyo sasa anasubiri kufungwa jela  baada ya ushahidi kudhibitisha kuwa ndiye aliyemuua Bi Jackeline Ngina Kitheka.

Vyombo kama neti ya mbu, pasi, taulo za kitanda na mashine ya kukausha nywele vilivyopatikana nyumbani kwa mshtakiwa baada ya kuibwa kutoka nyumba ya marehemu ndivyo vilivyothibitisha kesi ya mauaji.

Mahakama Kuu mjini Mombasa ilimpata Waliaula na hatia ya kumuua kikatili mfanyabiashara huyo ambaye alikuwa akijiandaa kufunga ndoa na mchumba wake raia wa Uingereza, Harry Harrington.

Ingawa hakukuwa na ushahidi wa moja kwa moja, mahakama ilitegemea msururu wa matukio, mashahidi na vielelezo vilivyopatikana kwa nyumba ya mfanyabiashara huyo ambako Waliaula alikuwa ameweka baadhi ya vyombo hivyo kama dhamana ya mkopo.

“Vyombo vilivyopatikana vilikuwa mali ya marehemu, na ndivyo vilivyomhusisha Waliaula na mauaji haya,” ilisema mahakama, ikiongeza kuwa ushahidi kuhusu mazingira ya mauaji uliwasilishwa kwa uthabiti.

Scholastica Maghoha, shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka, alieleza mahakama kuwa Waliaula alikuwa mpenzi wake tangu Machi 2020, na walikuwa wakiishi pamoja Mtwapa kabla ya kuhamia Mombasa.
Alisema siku moja polisi walimpigia simu, na alipowaonyesha baadhi ya vitu alivyokuwa ameletewa na mshukiwa, aligundua baadaye vilitoka kwa marehemu Ngina.