Waandishi wahimizwa kutumia data wanaporipoti habari
Na LAWRENCE ONGARO
KUHIFADHI data za maswala muhimu kunahitajika ili kupata ukweli halisi wa jinsi mambo yalivyo.
Maafisa wa serikali kadha; kutoka Kaunti ya Nairobi, Kiambu, na Kajiado, walihudhuria kikao cha kujadili hali za wanawake kwenye kongamano la National Data-Driven Advocacy for Gender Equality lililoandaliwa katika mkahawa wa Maanzoni Lodge, Kaunti ya Machakos.
Mkurugenzi wa shirika la Groots Kenya linalojishughulisha zaidi na kutetea haki za wanawake mashinani Bi Fridah Githuku, alisema mkutano huo ulifana kwa sababu waandishi wa habari wapatao 30 walipata taswira bora kuhusu data za maswala muhimu ya kijamii.
“Nina matumaini ya kwamba waandishi wa habari wataangazia maswala mengi waliyoelezwa kuhusu changamoto kadha zinazoshuhudiwa katika jamii,” alisema.
Baadhi ya mambo muhimu yaliyojadiliwa kwa kina ni kuhusu umiliki wa vipande vya ardhi kwa wanawake wajane, na kadhia ya wasichana kuozwa wakiwa wadogo.
Maafisa wa serikali waliohudhuria hafla hiyo walielezea kwa kina data halisi za maswala hayo katika sehemu husika hapa nchini.
Serikali inahitaji kutafuta mbinu ya kushinikiza wale wanaotumia vibaya wafanyakazi; hasa wanaofanya za sulubu kuwalipa angalau pesa kiasi za kuwawezesha kukidhi mahitaji bila ugumu.
Mkutano ulijadili jinsi ambavyo watu wengi wamenyanyaswa; hasa wanawake ambapo imedaiwa hufanya kazi muda wa saa nyingi licha ya changamoto tele zilizopo.
Hafla hiyo ilijadili mengi kuhusu wanawake na wasichana ikidaiwa hukosa kumiliki hatimiliki za vipande vya ardhi kutokana na maswala ya utamaduni.
Kulingana na mkutano huo, ilibainika kuwa wasichana wadogo chini ya umri wa miaka 15 hukeketwa bila hiari yao. Ilielezwa kwamba kitendo hicho bado kinaendelea kisiri bila serikali kujua.
Kulingana na data ya kiafya mwaka wa 2014 asilimia 27.4 ya wasichana waliolewa chini ya umri wa miaka 16 ikilinganishwa na 1989 ambapo wasichana asilimia 44.5 walioolewa.
Utafiti huo uliyoendeshwa na Shirika la Groots Kenya umebainisha kuwa Kaunti ya Kakamega asilimia 84 ina wafanyakazi wengi wanawake wasiolipwa chochote huku wakifanya kazi za sulubu ikilinganishwa na asilimia 16 ya wanaume wanaoedesha kazi ya bwerere bila malipo.
Katika Kaunti ya Kiambu asilimia 80 ya wanawake ndio hufanya kazi ya sulubu nao wanaume wakiwa ni asilimia 20.
Wananchi wamehimizwa kufanya juhudi kuzuru afisi za serikali katika jumba la GPO, ili kutazama data tofauti zinazoangazia maswala mengi ya serikali.
“Afisi hizo ziko wazi kwa mwananchi yeyote ambaye angetaka kujijulisha mengi kuhusu jambo lolote lile kuhusu data kwa mambo ya serikali,” alisema Mkurugenzi huyo wa Groots Kenya.
Waandishi wa habari walipewa changamoto kuhakikisha ya kwamba wamezuru sehemu kadha mashinani na kufanya juhudi kuandika habari kuhusu yanayokumba jamii.
Mfano wa maswala hayo ulikuwa ni ndoa za mapema, wanawake kukosa haki zao hasa mashinani, na maswala ya ukeketati kwa wasichana.