Habari

Waasisi wa Handisheki

March 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

MUAFAKA kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, unatimiza mwaka mmoja leo Jumamosi huku ikibainika kuwa ulifanikishwa na watu wa familia zao mbili, shinikizo za jamii ya kimataifa na kwa kuepuka wandani wao waliokuwa na misimamo mikali.

Ni watu wa familia ya Rais Kenyatta ambao walikata kauli kupatanisha vigogo hao wawili wa kisiasa na wakaweka suala hilo kuwa la kibinafsi. Familia zote zilikubaliana kuweka juhudi hizo kuwa siri hadi mwisho.

Akizungumza na gazeti moja la humu nchini, kakake Bw Odinga, Dkt Oburu Odinga, alifichua kwamba ni watu wachache wa familia zote mbili waliohusika kupatanisha viongozi hao.

“Tulijua halikuwa jambo la mzaha na tulikuwa makini sana. Ni watu wachache waliofahamu na ninafikiri ndio sababu tulifaulu,” Bw Oburu aliambia gazeti hilo.

Na hili kudhihirisha halikuwa jambo la mzaha, inasemekana watu wa karibu wa familia ya Rais walifanya ziara za siri katika boma la Bw Odinga mtaani Karen kabla ya vinara hao kukubali kukutana.

Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga wakati wa kupeana salamu za maridhiano Machi 9, 2018. Picha/ Maktaba

Wengine kutoka familia ya Bw Odinga waliomshawishi kuzungumza na Rais Kenyatta ni mkewe Ida.

Kiongozi huyo wa chama cha ODM aliandamana na binti yake Winnie katika fisi ya rais Harambee House, Nairobi walipotangazia nchi muafaka wao.

Baada ya tangazo hilo, watu wa familia ya Rais Kenyatta wakiongozwa na ndugu yake Muhoho Kenyatta walianza kumchangamkia Bw Odinga.

Bw Muhoho aliyezuru Bondo kwa mara ya kwanza alikiri kwamba anamuunga kiongozi huyo wa upinzani kwa sababu ya handisheki.

Binamu wa Rais Kenyatta, Ngengi Muigai na dada yake seneta Beth Mugo pia walimtembelea Bw Odinga baada ya handisheki.

Wakati wa mazungumzo hayo, viongozi hao walikubaliana kuwa hawangehusisha washirika wao wa kisiasa ili yaweze kufaulu.

Washirika wa Bw Odinga walikuwa wakisisitiza kwamba hawakumtambua Uhuru kama rais nao wale wa Jubilee walikuwa wakishikilia kuwa hawangejadili uchaguzi isipokuwa maendeleo pekee.

Baada ya kupiga hatua kwenye mazungumzo, inasemekana Bw Odinga aliwadokezea baadhi ya wandani wake katika upinzani lakini hakuwapatia maelezo ya waliyokubaliana.

Walipotangaza muafaka wao, alikuwa ameandamana na mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohammed.

Jamii ya kimataifa iliingiwa na hofu baada ya Bw Odinga kujiapisha kuwa rais wa wananchi na kushinikiza pande zote mbili kushiriki mazungumzo ili kuondoa taharuki iliyokuwa imetanda nchini.

“Ninaamini jamii ya kimataifa hasa, serikali ya Amerika ilihusika (kupatanisha Rais Kenyatta na Bw Odinga),” mbunge wa Westlands, Tim Wanyonyi wa chama cha ODM aliambia Taifa Leo mnamo Ijumaa.

Shinikizo

Kulingana na wadadisi, japo viongozi hao wamekuwa wakisema walitafutana na kuamua kuzika tofauti zao baada ya mazungumzo, kulikuwa na shinikizo kutoka jamii ya kimataifa waweke maslahi ya nchi mbele kuliko ya kisiasa.

“Ilikuwa wazi kwamba nchi ilikuwa imegawanyika na tuliamua ni lazima tuweke kando tofauti zetu na kushiriki mazungumzo kwa lengo la kuunganisha nchi,” Bw Odinga alisema.

Bw Odinga alisema ilichukua juhudi za washauri wenye nia njema kumpatanisha na Rais Kenyatta japo kwa mwaka mmoja sasa amekataa kufichua waliowapatanisha.

Mnamo Alhamisi, Bw Odinga alifichua kuwa walijadiliana kwa muda kabla ya kuamua kuweka makubaliano yao kwenye maandishi.

“Halikuwa suala la siku moja. Tulijadiliana kwa muda kabla ya kuamua kuandika tuliyokubaliana,” Bw Odinga alisema kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio.