Habari

Wabunge 10 hatarini

October 8th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JOSEPH WANGUI

WABUNGE wanane pamoja na maseneta wawili wapo katika hatari ya kupoteza viti vyao.

Hii ni kufuatia uamuzi uliotolewa Jumatano na Mahakama Kuu ya Nairobi.

Jaji Weldon Korir alitoa uamuzi uliosema kuwa diwani anayehudumu haruhusiwi kisheria kuwania kiti cha ubunge kabla ya kujiuzulu rasmi kwa njia ya maandishi.

Akifutilia mbali uchaguzi wa Mbunge wa Gatundu Kaskazini Wanjiku Kibe, Jaji Korir alishikilia kwamba kisheria mbunge huyo hakufaa kuwania wadhifa huo kabla ya kujiuzulu kutoka cheo chake cha diwani.

Jaji Korir aliagiza Naibu Msajili wa Mahakama kuwasilisha uamuzi wake kwa Spika wa Bunge la Taifa ili atangaze kiti hicho cha Gatundu Kaskazini kuwa wazi. Hatua hiyo itapelekea kuandaliwa kwa uchaguzi mdogo katika eneobunge hilo.

Kabla ya kuchaguliwa kwenye uchaguzi mkuu wa 2017 kama mbunge, Bi Kibe alikuwa diwani mteule katika bunge la Kaunti ya Kiambu.

Mahakama ilishikilia kwamba mbunge huyo na Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) walishindwa kufuata kifungu cha sheria kwenye Katiba kinachomzuia MCA kuchaguliwa kama mbunge akiwa bado madarakani.

Kwa mujibu wa Katiba, diwani yeyote anayepania kuwania kiti cha ubunge lazima aandike barua ya kujiuzulu kwa spika wa bunge la kaunti, miezi sita kabla ya siku ya uchaguzi.

Uamuzi huo wa Jaji Korir huenda ukawafanya baadhi ya wabunge na maseneta waliokuwa madiwani ama maspika kabla ya uchaguzi wa 2017 kupoteza nyadhifa zao.

Baadhi yao ni Mary Waithira Wamaua (Maragua), Fred Ouda (Kisumu ya Kati), Catherine Waruguru (Laikipia) na Joyce Korir (Bomet).

Wengine ni Glady Mbeyu (Kilifi), Asha Mohamed (Mombasa) na Patrick Mariru (Laikipia Magharibi).

Maseneta Cleophas Malala (Kakamega) na Susan Kihika (Nakuru) pia wamo kwenye hatari.

Bw Mariru na Bi Kihika walikuwa maspika wa mabunge ya Laikipia na Nakuru mtawalia.

Akitoa uamuzi wake kuhusu kura ya eneobunge la Gatundu Kaskazini, Jaji Korir alisema kuwa uchaguzi huo ulikiuka kanuni ya uchaguzi na Katiba ya Kenya, kwa hivyo Bi Kibe alichaguliwa kwa njia haramu.

Aliyekuwa mbunge wa eneo hilo Kung’u Waibara, ambaye aliwasilisha kesi hiyo kortini, alisema kwenye utetezi wake kuwa kufikia Agosti 8, 2017, Bi Kibe hakuwa amejiuzulu kama diwani mteule.

Mnamo Juni, 2017, jina la mtangazaji huyo wa zamani lilichapishwa na IEBC kama mwaniaji wa kiti hicho cha ubunge kupitia chama cha Jubilee.

Korti ilikubali utetezi wa Bw Waibara kwamba Bi Kibe alikuwa akiendelea kushikilia wadhifa huo wa mbunge kwa njia haramu kwani hatua hiyo inakiuka Katiba na haifuati sheria, uwajibikaji na uwazi.

“Ingawa alikuwa na nafasi ya kujiuzulu, hakuna ushahidi kwamba Bi Kibe alifanya hivyo kabla ya uteuzi wa chama cha Jubilee. Ukweli ni kwamba Bi Kibe kufikia wakati wa uteuzi wa Jubilee alikuwa diwani ambaye alikuwa akilipwa mshahara,” akasema Bw Waibara kwenye kauli zake kwa korti.

Baada ya uamuzi huo, Bi Kibe alisema atakata rufaa akieleza kwamba ulikuwa na dosari.

Wakili wake, Omwanza Ombati, alisema jaji Korir alikiuka kanuni kwa kusikiza kesi ambayo iliwasilishwa miaka mitatu baada ya uchaguzi, kinyume na sheria inayosema kesi za kupinga uchaguzi inafaa ziwasilishwe na kukamilishwa katika muda wa miezi sita baada ya uchaguzi.