HabariHabari za Kitaifa

Wabunge kumwomboleza Raila mnamo Alhamisi, Spika Wetangula akiwataka wavalie mavazi meusi  

Na CHARLES WASONGA October 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

WABUNGE mnamo Alhamisi, Oktoba 16, 2025 watapata nafasi ya kumwombolewa Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga aliyefariki Oktoba 15, akipokea matibabu nchini India.

Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula Jumatano aliwaagiza wabunge kuvalia mavazi meusi akiwaambia “mje mkiwa na sura za huzuni”.

“Napendekeza kwamba sote tuvalie mavazi meusi katika kikao hicho kitakachoanza saa nne asubuhi. Kwa wale ambao hawana mavazi meusi, tafadhali myanunue baada ya kikao hiki. Nao wenzetu wa kike waje na riboni kuashiria maombolezo,” akasema.

“Katika kikao hicho, kila mbunge atapata nafasi ya kumwomboleza Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga baada ya habari kuhusu kifo chake kutangazwa rasmi na Rais William Ruto. Sote tuwe na sura ya maombolezo,” Bw Wetang’ula akaeleza.

Spika, pia, aliamuru kwamba kikao cha alasiri cha bunge la kitaifa Alhamisi kitaanza saa nane na nusu hadi usiku wa manane (saa sita za usiku).

Bw Wetang’ula alimtaja Raila kama kiongozi ambaye sifa zake zilizagaa kote nchini ambako alikuwa na wafuasi.

“Waziri Mkuu wa zamani alikuwa mkubwa kuliko Kisumu. Alihusudiwa kuanzia Vanga hadi Lodwar. Na sifa zake zilienea hata nje ya mipaka ya taifa la Kenya,” akasema.

Kiongozi wa Wengi, Kimani Ichung’wah aliwasilisha rasmi hoja ya kuahirishwa kwa kikao cha Jumatano ili kutoa nafasi kwa wabunge kuomboleza Hayati Mzee Odinga, kiongozi wa ODM.

Hoja hiyo iliungwa mkono na kiongozi wa wachache Junet Mohamed ambaye alionekana kujawa na huzuni.

Kufuatia kuahirishwa kwa kikao cha Alhamisi, mjadala kuhusu miswada kadhaa ilisitishwa.

Baadhi ya miswada hiyo ni: Mswada wa Pareto, Mswada wa Huduma za Maktaba ya Kitaifa ya 2024, Mswada Kuhusu Afya ya Watoto Wachanga na Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Sekta ya Majani Chai.