Wabunge na maseneta wazimwe kuwa mawakili – Uhuru
Na BENSON MATHEKA
RAIS Uhuru Kenyatta Alhamisi aliwakemea maseneta na wabunge wanaofika kortini kuwakilisha washukiwa, akisema wanafaa kuamua ikiwa wanataka kuwa watumishi wa umma au kuhudumu kama mawakili.
Akionekana kuwalenga maseneta na wabunge waliofika kortini kumwakilisha Gavana wa Nairobi Mike Sonko aliposhtakiwa kwa ufisadi Jumatatu, Rais Kenyatta alisema maafisa wa umma hawafai kujihusisha na taaluma zao za kibinafsi wakiendelea kuhudumu.
“Mtu hawezi kuwa mbunge katika bunge la kitaifa au kaunti na wakati huo huo aendelee kuhudumu kama mwanasheria iwe ni kwa malipo au la,” alisema Rais Kenyatta akihutubia taifa kwenye sherehe za 56 za kuadhimisha Jamhuri Dei.
Maseneta Kipchumba Murkomen na Mutula Kilonzo Junior pamoja na mbunge wa Makueni, Daniel Maanzo walikuwa miongoni mwa mawakili 12 waliomwakilisha Bw Sonko.
Seneta wa Siaya James Orengo, mwenzake wa Nyamira Okongo Omongeni na mbunge wa Rarienda Otiende Amollo ni miongoni mwa mawakili ambao wamekuwa wakifika kortini kuwakilisha washukiwa hasa wanasiasa.
Rais Kenyatta pia aliingilia mzozo wa Tume ya Huduma ya Walimu (TSC) na Katibu Mkuu wa chama cha Knut, Wilson Sossion kwa kusema mwalimu hawezi kuteuliwa mwanasiasa na kisha aendelee kufunza.
“Mwalimu katika utumishi wa umma hawezi kuwa na mguu mmoja darasani na mwingine bungeni,” akasema.
Alisema wataalamu wanaokubali kuwa watumishi wa umma wanafaa kuacha kazi zao za kibinafsi na kutumia nguvu zao na wakati wao wote katika kazi zao za serikali bila kuonekana kuwa wanazitumia kuendeleza maslahi yao ya kibinafsi.
“Je, ni haki na sawa kwa wabunge wanaosimamia pesa za umma na kuchunguza mahakama kufika kortini kama mawakili?” alihoji Rais Kenyatta.
Rais aliagiza Mwanasheria Mkuu, Paul Kihara kuharakisha mswada wa sheria utakaohakikisha kuwa watumishi wa umma hawataweza kutumia afisa zao kujinufaisha.
“Vita dhidi ya ufisadi vitaendelea hadi tubandue kabisa wale wanaotumia nyadhifa zao kujinufaisha. Hakuna hakimu, jaji au afisa yeyote wa umma, ambaye ametumia vibaya ofisi yake ataruhusiwa kujificha nyuma ya uhuru uliotwikwa afisa yake,” alisema.
Alieleza kuwa amejitolea kuhakikisha kuwa Kenya itabaki nchi iliyoungana na ambayo raia wote wana haki sawa.