Habari

Wabunge sasa wategemea Mahakama ya Rufaa kuokoa hazina ya NG-CDF

Na SAMWEL OWINO January 7th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

WABUNGE bado wana matumaini kuwa Mahakama ya Rufaa itaokoa hatima ya Hazina ya Serikali ya Kitaifa ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (NG-CDF) baada ya Mahakama Kuu kuitangaza kuwa kinyume cha Katiba mwaka wa 2024.

Mnamo Septemba 2024, Mahakama Kuu ilitangaza sheria ya NG-CDF inakiuka kanuni ya kutenganisha mamlaka na kwamba Bunge halikuhusisha Seneti wakati wa kutungwa kwa sheria hiyo.

“Sheria ya Hazina ya Serikali ya Kitaifa ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (NG-CDF) kama ilivyorekebishwa mwaka wa 2022 na 2023 inatangazwa kuwa kinyume cha Katiba, na miradi, mipango na shughuli zake zote zitasitishwa kuanzia saa sita usiku wa Juni 30, 2026,” jopo la majaji lilisema.

Hata hivyo, Bunge la Kitaifa lilikata rufaa dhidi ya uamuzi huo, huku Mahakama ya Rufaa ikitarajiwa kutoa uamuzi wake Februari 6, 2026.

Wakiongozwa na Mbunge wa Rarieda, Dkt Otiende Amollo, pamoja na George Murugara (Tharaka), Peter Kaluma (Homa Bay Town) miongoni mwa wengine, Bunge la Kitaifa lina matumaini kuwa Mahakama ya Rufaa itaokoa hazina hiyo dhidi ya kufutwa kuanzia Juni 30 mwaka huu.

Akitoa taarifa kuhusu suala hilo bungeni, Dkt Amollo, aliwaeleza wabunge wenzake kuhusu hali ya rufaa iliyowasilishwa katika Mahakama ya Rufaa, akisema ana matumaini kuwa makosa ya kisheria yaliyofanywa na Mahakama Kuu yatasahihishwa.

“Ninaamini tutaishawishi Mahakama kurekebisha makosa ya sheria yaliyofanywa na Mahakama ya chini. Tuliomba Mahakama itoe uamuzi wake kwa wakati, tukizingatia kuwa athari ya uamuzi wa Mahakama Kuu ni saa sita usiku wa Juni 30, 2026,” alisema Dkt Amollo.

“Pia tulikumbusha Mahakama kuwa itakuwa dhuluma kubwa ikiwa mchakato wa bajeti utaanza kabla ya hukumu kutolewa. Tunafuraha kuripoti kuwa Mahakama ilisikiliza ombi hilo na ikaweka tarehe ya kutoa uamuzi kuwa Februari 6, 2026, ambayo ni muda muafaka na wa mapema iwezekanavyo,” aliongeza.

Mbunge huyo wa Rarieda aliongeza kuwa wabunge wanataka kuona hazina ikiendelea kustawi.

“Hii ni hazina ya Serikali ya Kitaifa inayosimamiwa kwa uhuru na kamati husika. NG-CDF haiwasaidii wabunge binafsi, bali inawanufaisha wapiga kura wao,” alisema.

Kwa upande wake, Bw Murugara alisema Bunge limefanya wajibu wake na sasa ni jukumu la Mahakama kutoa uamuzi wake huru.

“Hatuwezi kusema matokeo yatakuwa vipi kwa sababu hakuna wakili anayeweza kutoa uhakika katika kesi yoyote. Kama kesi nyingine zote, hakuna uhakika. Tulifanya tuwezavyo,” alisema.

Aliongeza kuwa jopo la majaji liliuliza maswali muhimu ambayo wanaamini walijibu vizuri, lakini wakaacha uamuzi mikononi mwa Mahakama.

Mbunge wa Suba Kusini, Caroli Omondi, alisema huku Bunge likisubiri uamuzi wa Mahakama, linapaswa kuendelea kupanga na kujumuisha mgao wa NG-CDF katika Mwaka wa Fedha wa 2026/2027.

“Hakuna hazina iliyo na faida nyingi kwa watu wengi kama NG-CDF, lakini imeeleweka vibaya kwa sababu zisizo sahihi. Mgao wa NG-CDF unapaswa kuzingatiwa; tusiruhusu juhudi zetu zipotee,” alisema Bw Omondi.

Baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu, Bunge la Kitaifa lilianza kushughulikia mapungufu ya kisheria yaliyobainishwa.

Tangu wakati huo, Bunge limepitisha Mswada wa Marekebisho ya Katiba ya Kenya, 2025, unaolenga, miongoni mwa mambo mengine, kuingiza NG-CDF moja kwa moja katika Katiba.

Sheria ya CDF ilitungwa mwaka wa 2003 na baadaye kurekebishwa mwaka wa 2007, ikieleza kuwa serikali inafaa kutenga angalau asilimia 2.5 ya mapato ya mwisho yaliyokaguliwa na kuidhinishwa na Bunge la Kitaifa, kuelekezwa katika hazina hiyo kwa matumizi katika maeneo bunge.