Wabunge wa Kaskazini Mashariki wapendekeza kukamatwa kwa Ngilu
Na CHARLES WASONGA
WABUNGE kutoka eneo la Kaskazini Mashariki wamemkashifu Gavana wa Kitui Charity Ngilu kwa kile walichodai ni kuchochea chuki dhidi ya watu wa jamii ya Wasomali na Waislamu na wakata akamatwe.
Walisema watu wa jamii ya Kisomali wana haki na kuishi popote nchini Kenya bila kuomba ruhusa kutoka kwa yoyote.
“Hii ndiyo maana tunamtaka Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti kumchunguza kwa kuchochea wenyeji wa Kitui dhidi ya wafugaji kutoka jamii ya Wasomali na ambao wako huko kutafuta lishe kwa mifugo wao,” Mbunge wa Aldas Aden Keynan akasema kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge Jumatano.
Aliandamana na wenzake; Ahmed Kolosh (Wajir Magharibi), Bashir Abdullahi (Mandera Kaskazini), Mohamed Garane (Lagdera), Omar Shurie (Balambala), Abdi Mule (Lafey) na Ali Wario (Bura).
Wabunge hao walikuwa wamekerwa na kanda ya video ambayo imekuwa ikisambaa mitandaoni yeye sauti inayodaiwa kuwa ya Bi Ngilu akiwahimiza wenyeji wa Kitui kuchukua silaha na kushambulia wafugaji ambao wamevamia mashamba yao.
Huku wakionekana pia kutenda kosa ambalo wanadai Ngilu ametenda, wabunge hao walitisha kuchukua “hatua kali dhidi ya Ngilu” ikiwa serikali haitaamuru akamatwe na ashtakiwe.
Lishe na malisho
Bw Bashir, maarufu kama Meja Bashir, alimkashifu Bi Ngilu kwa kuleta migawanyiko baina ya Waislamu na wale ambao sio Waislamu katika Kaunti ya Kitui kwa sababu ya lishe.
“Inasikitisha kuwa kiongozi wa hadhi ya Gavana anaweza kutoa matamshi kama hayo. Bi Ngilu alitoa matamshi ya kuchochea chuki na hivyo anafaa kukamatwa na kufunguliw mashtaka,” akasema.
Bw Keynan aliongeza kuwa Kenya inatawaliwa na Katiba na sheria nyinginezo na Gavana Ngilu anafaa kuwajibikia matamshi yake.
“Ikiwa kweli taifa hili linaheshimu utawala wa sheria, basi Gavana Ngilu anafaa kukamatwa ili iwe funzo kwa viongozi wengine wenye mazoea ya kutoa matamshi kama hayo,” akasema.
Sauti kwenye kanda hiyo inawahimiza vijana kuchukua silaha na kupambana na ‘wahalifu’ waliovamia kijiji cha Mathu kaunti ya Kitui. Ilidaiwa kuwa watu hao walikuwa ni sehemu ya wafugaji kutoka kaunti za eneo la Kaskazini Mashariki ambao walikuwa wakisaka lishe kwa mifugo wao kutokana na kiangazi kinachoshuhudiwa makwao.
Mwaka 2018 viongozi wa kisiasa kutoka Kiambu walishinikiza kukamatwa kwa Bi Ngilu kwa madai kuwa alichochea wakazi kuteketeza malori ambayo yalikuwa yakisafirisha makaa kupitia Kaunti ya Kitui.