Wabunge wa Kenya waduwazwa 3-1 na wenzao wa Uturuki
Na GEOFFREY ANENE
BUNGE FC imepoteza raundi ya kwanza ya mechi ya kirafiki dhidi ya Uturuki baada ya kulimwa 3-1 katika klabu ya michezo ya Parklands jijini Nairobi, Jumanne.
Vijana wa kocha Sylvester Ochola walipata bao la kufutia machozi kutoka kwa Seneta wa kaunti ya Kakamega, Cleophas Malala dakika tatu kabla ya kipenga cha mwisho kilie.
Katika mchuano huu wa kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya mataifa haya, Uturuki iliizidi Bunge na chenga za maudhi na pasi za uhakika katika uwanja telezi baada ya mvua kunyesha jijini Nairobi mapema asubuhi.
Bunge haikuwa imetulia kabla ya kujipata bao moja chini baada ya Ibrahim Halil Yildiz kucheka na wavu dakika ya kwanza.
Kenya ilipata nafasi murwa dakika chache baadaye, lakini Mbunge wa Rarieda Otiende Amolo hakukamilisha vyema ikabu kutoka kwa Mbunge wa Homa Bay, Peter Kaluma.
Uturuki kisha ilipata nafasi ya kuimarisha uongozi wake dakika mbili kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika pale Bunge ilifanya masihara ndani ya kisanduku chake na kutunuku wageni hao penalti.
Yildiz alivuta mkwaju huo kwa mguu wake wa kushoto, lakini kipa Jimmy Okwiri alikuwa macho na kuipangua. Hata hivyo, walinzi wa Bunge hawakumakinika na Sarikaya akahakikisha Uturuki haipotezi nafasi hiyo na kuiweka mabao 2-0 juu.
Huku muda ukiipa Bunge kisogo, Mbunge wa Nyali, Mohammed Ali alivuta krosi nzuri, lakini Victor Munyaka (Machakos Town) akapiga mpira hafifu uliodakwa na kipa.
Sarikaya, ambaye alikuwa mwiba kwa timu ya Kenya kwa chenga zake na kasi pembeni kushoto, alipachika bao la tatu dakika ya 53 baada ya Okwiri na wenzake kuzembea.
Malala aliondolea Bunge aibu ya kumaliza mechi bila bao alipofuma wavuni ikabu safi kutoka pembeni kulia. Bunge ilipata frikiki hiyo baada ya nahodha Daniel Wanyama (Webuye West) kuangushwa nje ya kisanduku.
Timu hizi zinafanya mpango wa kuwa na mechi ya marudiano katika mji wa Antalya ama Istanbul. Bunge imeapa kulipiza kisasi ugenini.