Wabunge waamuru SRC kuwasilisha taarifa kuhusu mishahara ya maafisa wengine wa serikali
Na CHARLES WASONGA
BUNGE la Kitaifa Jumanne liliendeleza vita vyake na Tume ya Kukadiria Mishahara na Marupurupu ya Wafanyakazi wa Umma (SRC) kwa kuipa makataa ya siku 14 kuelezea ni kwa nini kuna utofauti kati ya mishahara ya maafisa wakuu wa serikali na watumishi wengine wa umma.
Hatua hiyo ilitokana na swali ambalo liliulizwa na Mbunge wa Homa Bay Mjini Peter Kaluma aliyelalamika kwamba tume hiyo haijaweka wazi viwango vya mishahara na marupurupu ambayo maafisa wengine hupokea kama inavyofanya kwa malipo ya wabunge.
Katika swali lake Bw Kaluma anataka SRC kutoa vigezo ilivyotumia kubaini mishahara, marupurupu, bima ya afya, mkopo wa nyumba na manufaa mengine ambapo maafisa wakuu wa serikali na wanachama wa tume za kikatiba hupokea.
“Kando na hayo, ninataka SRC kutoa maelezo kuhusu mishahara na marupurupu ambayo manaibu wa mawaziri (CAS) wanapokea, na mapato ya wakurugenzi wakuu wa mashirika ya serikali. Vilevile tume hiyo ieleze kuwa mishahara na marupurupu yao yamechapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali,” akasema Bw Kaluma ambaye ni mbunge wa chama cha ODM.
Akaongeza: “Tunataka SRC kueleza ni kwa nini kila mwenyekiti wa tume za kikatiba hupokea Sh50,000 kama marupurupu ya vikao kimoja na Sh40,000 kwa kila kikao kwa wanachama wa kamati. Na tume hiyo iseme ni kwa nini ikiwa marupurupu ya vikao ya Sh5,000 ya wabunge – kila mmoja – huangaziwa zaidi kuliko yale ambayo maafisa wengine hupokea.”
Majibu katika maandishi
Alimtaka Spika Justin Muturi kuamuru kwamba SRC itume majibu kwa maandishi “ili Wakenya waweze kuelewe ukweli kuhusu suala hili ambalo limeibua joto katika ulingo wa siasa.”
Hapo ndipo Bw Muturi aliamuru hivi: “Swali hili liwasilishwe kwa SRC na waweze kutoa majibu kwa bunge ndani ya siku 14 kuanzia leo (jana Jumanne).”
Wabunge wamekuwa wakivutana na SRC kuhusu hatua Tume ya Huduma za Bunge (PSC) kuamua kuwalipa viongozi hao marupurupu ya nyumba ya Sh250,000 kila mwezi.
SRC ilipinga hatua hiyo ikidai iliidhinisha bila ushauri wake, inavyohitajika kikatiba; ndiposa ikawailisha kesi mahakamani kupinga malipo hayo.