Wabunge waapa kung'oa Rotich kwa kuongeza bei ya mafuta
Na MWANDISHI WETU
MABUNGE sasa wameapa kumtima Waziri wa Fedha Henry Rotich baada ya kusisitiza kutoza Wakenya ushuru zaidi wa mafuta licha ya bunge kutupa pendekezo hilo.
Baadhi ya wabunge wameapa kuwasilisha Bungeni mswada wa kura ya kutokuwa na imani na Bw Rotich kutokana na hatua hiyo.
Seneta Cleopas Malala na mbunge maalum Godfrey Osotsi walisema ilikuwa kinyume cha Katiba kwa Waziri Rotich kupuuza uamuzi wa Bunge.
“Kwa mara nyingine Wakenya ambao tayari wamelemewa na mzigo mkubwa wa ushuru watahisi uchungu wa mikopo zaidi kwa upande wa serikali huku bei ya mafuta ikizidi kupanda kwa sababu Bw Rotich amepuuza Bunge,” alisema Bw Osotsi jana.
“Bunge ndiyo taasisi ambayo imepewa mamlaka na Katiba kutunga sheria. Uamuzi wa Bunge ni wa mwisho. Kilichokuwa kimesalia ni kwa rais kutia sahihi au kukataa Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Fedha 2018. Mbona waziri anaharakisha kutekeleza sheria hiyo?” aliuliza.
Mbunge wa Ganze Teddy Mwambire na mwenzake wa Magarini Bw Michael Kingi walisema hatua hiyo ni kinyume cha sheria za bunge.
Kutokana na hilo, walimtaka Bw Rotich achukuliwe hatua kali kutokana na kukiuka maamuzi ya bunge ambalo ni muhimu kama macho ya Wakenya.
“Bw Rotich lazima awajibikie Wakenya vizuri. Wakati bunge lilipoamua kwamba kuongeza ushuru wa ziada kutaathiri Wakenya, yeye hakufaa kamwe kuendelea mbele na mpango huo. Lazima akamatwe kwa kwenda kinyume cha sheria za taifa hili,” akasema Bw Mwambire.
“Sio vyema kwa waziri huyu kuamua kupuuza maamuzi ya bunge na kuendelea mbele na mpango wake. Kama wabunge, ni lazima tumuite bungeni aeleze ni kwa nini aliamua kuchukua hatua hiyo,” akasema Bw Kingi. Seneta Malala alishauri wabunge na maseneta kupiga kura ya kutokuwa na imani dhidi ya Bw Rotich kwa kusema waziri huyo alikiuka uamuzi wa Bunge.
Licha ya pingamizi nyingi kutoka kwa wananchi, Mamlaka ya Kukusanya Ushuru nchini (KRA) jana ilitangaza kuwa ingeanza kutekeleza sheria hiyo kuanzia jana.
“KRA inatangazia umma, wauzaji wa mafuta, wasambazaji na wauzaji rejareja kuwa ushuru wa VAT utaanza kutozwa kwa bidhaa zote za mafuta kwa asilimia 16 kuanzia Septemba 1,” ilisema KRA katika taarifa katika vyombo vya habari.
Mapema wiki jana, Bunge liliahirisha utekelezaji wa sheria hiyo kwa miaka miwili kwa lengo la kuwakinga wananchi.
Hata hivyo, mswada wa marekebisho hayo haukutiwa sahihi na Rais Uhuru Kenyatta kabla ya kuelekea Uchina kwa mkutano, hali ambayo ilitoa nafasi kwa KRA kutekeleza sheria hiyo.
“Mabadiliko hayo yamo katika Sheria ya Fedha ya 2013 ambayo ilirefusha kipindi cha kuanza kutekelezwa kwa sheria kwa miaka mitatu,” ilisema KRA na kuongeza kuwa hali ya kutotekeleza sheria hiyo ilirefushwa tena kwa miaka miwili zaidi kutokana na Sheria ya Fedha ya 2016.
“Kutokana na hilo, VAT kwa bidhaa za petroli lazima sasa ianze kutekelezwa,” alisema kamishna mkuu wa KRA John Njiraini katika taarifa hiyo.
Baraza la Maimamu na Wahubiri (CIPK) eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa jana lilitahadhrisha Waziri wa Fedha Henry Rotich dhidi ya kupuuza msimamo wa wabunge kuhusu bei ya mafuta ambayo inatarajiwa kupanda kutokana na uamuzi huo.
Viongozi wa baraza hilo walionya kuwa iwapo bei ya mafuta itapanda kutokana na ushuru wa mafuta bila shaka utakuwa mwanzo wa kupanda kwa gharama ya maisha nchini.
Mwenyekiti wa baraza hilo Sheikh Abubakr Bin alisema msimamo wa wabunge ni msimamo wa Wakenya wa tabaka la chini ambao wataathirika pakubwa na kupanda kwa bei ya mafuta.
“Waziri wa fedha anapaswa kujua kuwa wabunge wanatuwakilisha sisi wananchi wa tabaka la chini, iwapo waziri atatumia nafasi yake kushinikiza bei hiyo kupanda ajue vilio vya Wakenya vitakuwa katika kichwa chake,” alisema Sheikh Bin.
Kulingana na KRA, wauzaji wa mafuta, wasambazaji na wauzaji rejareja wanafaa kuandikisha kulipa ushuru huo kufikia kila tarehe ya 20 katika mwezi unaofuatia.
Kulingana na kamishna huyo, KRA imebuni mikakati ya kusaidia washikadau katika sekta ya mafuta kwa lengo la kuwawezesha kutekeleza sheria.
“Tumejadiliana na Tume ya Kudhibiti Kawi (ERC) kwa lengo la kuhakikisha kuwa imeratibu mashirika ya serikali kutekeleza sheria hiyo,” alisema.