Habari

Wabunge wajibu makombora ya Raila kuhusu hujuma kwa ugatuzi

Na SHABAN MAKOKHA April 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MZOZO wa kisiasa unatokota kati ya Kiongozi wa ODM Raila Odinga na wabunge, kufuatia matamshi yake akilaumu wawakilishi hao kwa kuhujumu ugatuzi kwa kujipatia fedha na kutwaa majukumu ya serikali za kaunti.

Akizungumza katika mazishi ya mlinzi wake wa miaka mingi George Oduor yaliyofanyika Siaya wiki jana, Bw Odinga alidai kuwa wabunge wamekuwa wakijaribu kudhibiti majukumu yaliyotengewa serikali za kaunti kikatiba, kama vile ujenzi na utengenezaji barabara na usimamizi wa shule.

“Wabunge ndio kikwazo kikubwa zaidi kwa fedha za ugatuzi kufikia kaunti,” alisema Bw Odinga, akiongeza kuwa ugatuzi utakuwa ajenda kuu katika uchaguzi mkuu wa 2027.

“Wanaouhujumu watakumbana na hasira za wananchi,” aliongeza.

Bw Odinga aliapa kuongoza kampeni dhidi ya wabunge wanaoendelea kuzuia au kuhujumu ugatuzi, huku akiwataka wazingatie majukumu yao ya kikatiba: kutunga sheria, kuwakilisha wananchi na kusimamia matumizi ya fedha.

Aidha, alikosoa Bunge la Kitaifa kwa kupunguza mgao wa fedha kwa kaunti. Alitoa mfano wa hivi majuzi ambapo Bunge lilipunguza pendekezo la mgao wa Sh415.9 bilioni lililoidhinishwa na Seneti na Tume ya Ugavi wa Mapato, hadi Sh391.1 bilioni.

Kauli ya Bw Odinga imezua kero kutoka kwa baadhi ya wabunge, akiwemo Mbunge wa Mumias Mashariki, Peter Salasya, ambaye alitetea jukumu la Bunge na kuwalaumu magavana kwa huduma duni mashinani.

“Kaunti nyingi zimeshindwa hata kujenga madarasa ya chekechea. Watoto bado wanasomea chini ya miti au kuketi sakafuni,” alisema Bw Salasya.

“Ni vipi tutawakabidhi mfumo mzima wa elimu ilhali hawawezi hata kuendesha shule za chekechea au vyuo vya kiufundi?”

Mbunge huyo pia aliwalaumu magavana kwa kutumia vibaya fedha na kuwanyima madiwani rasilmali muhimu kwa barabara za mashinani.

“Shirika la KeRRA limekuwa likifanya kazi nzuri ya kutengeneza barabara vijijini. Ndiyo maana tunataka barabara zote za mashinani ziendelee kusimamiwa na KeRRA,” aliongeza.

Wakati huo huo, magavana wameitaka Bunge kuharakisha kupitisha Mswada wa Ugavi wa Fedha za Ziada kwa Serikali za Kaunti mwaka 2025 wakionya kuwa ucheleweshaji zaidi utalemaza utoaji wa huduma.

Wakizungumza mbele ya Kamati ya Bajeti na Matumizi ya Fedha ya Bunge, Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa na mwenzake wa Homa Bay, Gladys Wanga, walisema kuchelewa kwa mswada huo kumesababisha mzozo na kupotea kwa ufadhili muhimu kutoka kwa wafadhili wa kimataifa.

“Mswada huu uliorekebishwa unarudisha mgao muhimu, lakini kuchelewa kupitishwa kwake kumedhoofisha uwezo wetu wa kutumia fedha ipasavyo,” alisema Bw Barasa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya Baraza la Magavana.

Mswada huo unapendekeza nyongeza ya Sh50.5 bilioni kwa kaunti. Wakati wa kikao hicho, mvutano wa kisheria kuhusu Hazina ya Matengenezo ya Barabara, ambapo Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Samuel Atandi, alitaka mazungumzo ya kitaifa kutatua tofauti zilizopo.