Wabunge wafungiwa afisi, vyoo KICC kutokana na malimbikizi ya kodi
WABUNGE Jumatatu walifungiwa nje ya afisi zao katika Jumba la Kimataifa la Mikutano la KICC kutokana na malimbikizi ya kodi ambayo sasa ni Sh50 milioni.
Pia walioathirika kutokana na utata kati ya KICC na Bunge ni wafanyakazi wa Tume ya Huduma za Bunge (PSC) ambao wana afisi zao katika jengo hilo.
Mnamo Jumatatu, Seneti iliwaambia wanachama wake kuhusu tukio hilo huku PSC ikimwaandikia Afisa Mkuu Mtendaji wa KICC, James Mwaura, kuhusu utata wenyewe.
Katika barua yake, Seneti iliomba wanachama wake watumie afisi zao ikiahidi kwamba deni hilo litalipwa kabla ya kutamatika kwa mwaka huu wa fedha.
“Habari za asubuhi maseneta. Nawafahamisha kuwa kutokana na malimbikizi ya kodi, usimamizi wa KICC umefungia afisi zetu na pia maegesho,” ikasema sehemu ya notisi.
“Kodi hiyo hulipwa na bunge na tumefahamishwa kuwa juhudi zinaendelea kushughulikia suala hili. Tunasikitikia usumbufu ambao suala hili umesababishia wafanyakazi,” ikaongeza.
PSC katika barua iliyoandikwa Mei 9 iliomba KICC iwaruhusu wabunge na wafanyakazi wengine waendelee kuitumia huku wakitafuta mbinu ya kushughulikia suala hilo. Barua ilinakiliwa kwa Spika Moses Wetang’ula ambaye ni mwenyekiti wa PSC.
Tume hiyo ina mkataba na KICC kuwapa wabunge makao na maegesho pamoja na wafanyakazi wao.
“Uhusiano huu umedumu kwa miaka mingi na PSC imekuwa ikitimiza wajibu wake japo wakati mwingine huwa inachelewa kutokana na kupunguzwa kwa pesa inayotengewa kwenye bajeti na pia hazina kuu kuchelewesha mgao,” ikasema barua hiyo.
Wabunge Jumatatu walipojaribu kuingia kwenye afisi zao walipata milango imefungwa huku usimamizi wa KICC pia ukiwafungia choo.
Taifa Leo ilipomfikia Bw Mwaura kuhusu utata huo, alisema alikuwa mkutanani na hangezungumza kuhusu suala hilo.
Kwenye bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2025/26, Bunge lilitengewa Sh42.5 bilioni ambapo Sh41.1 bilioni zilikuwa zimeelekezwa katika ulipaji wa mishahara na Sh1.4 bilioni kwa miradi ya maendeleo.