Habari

Wabunge wandani wa Ruto wamkaanga Kinoti

November 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE 40 wandani wa Naibu Rais William Ruto wamemshambulia vikali mkurugenzi wa Idara ya Upelekezi wa Jinai (DCI) George Kinoti kwa kile wamedai Jumanne anafufua kesi za ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007.

Wakiongozwa na Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen wabunge hao wa mrengo wa ‘Tangatanga’ wamesema Bw Kinoti anachochea uhasama miongoni mwa jamii zinazoishi Rift Valley kutimiza malengo ya “wakubwa” wake na kutaka kuzima ndoto ya Naibu Rais William Ruto ya kuingia Ikulu 2022.

“Lakini sisi kama wabunge tunaounga mkono amani na maridhiano tunatoa wito Wakalenjin, Wakikuyu, Wasomali, Waluo, Waluhya, Wakisii na jamii zingine zote zinazoishi Rify Valley kupuuzilia mbali njama hizo na waendelea kuishi kwa amani,” akasema Bw Murkomen.

Akaongeza: “Isitoshe, tunafanya kila tuwezalo kuhakikisha kwamba hakuna damu itamwagika tena Rift Valley kutokana na sababu za kisiasa. Kinoti na mabosi wake waelewe kuwa enzi hizo zimepita. Wasitumie makaburi ya waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 kuchochea mapigano tena katika eneo la Rift Valley.”

Akisoma taarifa ya pamoja ya viongozi hao, Seneta wa Nakuru Susan Kihika amemsuta Bw Kinoti na kudai kuwa anatumiwa na kuwatia Wakenya, haswa wale wa Rift Valley, woga ili kupitisha BBI kuwafaidi watu fulani katika siasa za urithi 2022.

“Bw Kinoti na wakubwa wake wanataka kuchochea hofu katika eneo la Rift Valley ili wakazi waunge mkono mradi wa kisiasa wenye kufaidi watu fulani. Tunajua nia yao ni kumharibia jina Naibu Rais William Ruto ili aonekane kama mchochezi wa vita asiyestahili kuwania urais 2022,” akasema Bi Kihika.

Wabunge hao wamemtaka Rais Uhuru Kenyatta kumzima Bw Kinoti wakisema anamharibia sifa wakati atakapoondoka afisini baada ya kukamilisha muhula wake wa pili uongozini.

“Kiongozi yeyote hukumbukwa na yale ambayo yatatendeka anapaoelekea kuondoka afisini lakini sio yale aliyoyatenda miaka ya kwanza baada ya kuingia mamlakani. Kwa hivyo, Rais Kenyatta asikubali Kinoti na mabwana wake waharibu rekodi ya uongozi wake,” akasema Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua.

Mnamo Jumatatu, Kinoti alisema serikali imeamuru afisi yake kuhakikisha kuwa ghasia zingine na vifo havitatokea tena nchini mnamo 2022 au miaka mingine.

“Acha wajaribu tena. Tutafuata ukweli na tutaandaa faili zote kuhakikisha wachochezi wote wanadhibitiwa. Hatutaki kuokota maiti mara nyingine,” Bw Kinoti akasema Jumatatu baada ya kushuhudia waathiriwa 150 wakiandikisha taarifa kuhusu “vitisho walivyopokea”.

Wengi wao walitoka maeneo ya Kiambaa, katika kaunti ya Uasin Gishu na Molo (Nakuru).

“Hivi karibuni mtaona matokeo ya shughuli hii. Tutawasaka na kuwaadhibu kwa mujibu wa sheria,” akasema Bw Kinoti.

Wabunge wa Tangatanga vile vile wamemtaka Rais Kenyatta kuhakikisha kuwa mapendekezo yaliyomo katika ripoti za Waki na Tume ya Ukweli, Haki na Maridhiano (TJRC) yanatekelezwa ili kusaidia kuponyesha makovu ya dhuluma za kihistoria.