Habari

Wabunge washtuka kubaini ni jamii mbili tu CBK

Na CHARLES WASONGA September 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

GAVANA wa Benki Kuu ya Kenya (CBK) Kamau Thugge jana alitolewa kijasho na wabunge baada ya kubainika kuwa, idadi kubwa ya wafanyakazi katika benki hiyo wanatoka jamii mbili kubwa nchini.

Wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Uwiano na Utangamano wa Kitaifa, wakiongozwa na mwenyekiti wao Abdi Yussufu Haji, walilalamika wakisema sio haki kwamba asilimia 44.8 ya jumla ya wafanyakazi 1,311 wanatoka katika jamii hizi mbili.

“Ni kinyume cha Katiba ya Kenya kwamba, asasi muhimu kama Benki Kuu ya Kenya haiwakilishi sura ya Kenya kwa misingi ya uajiri wa wafanyakazi. Haikubaliki kwamba jamii moja inashikilia asilimia 24.8 za nafasi za ajira ilhali ni asilimia ya 17. 7 ya Wakenya wanaotoka jamii hiyo. Mbona asilimia 20 ya nafasi zinashikiliwa na watu kutoka jamii inayowakilisha asilimia 13 ya idadi ya Wakenya? Hii sio haki” akafoka Bw Haji ambaye ni Mbunge wa Mandera Magharibi.

Kulingana na ripoti iliyowasilishwa na Dkt Thugge mbele ya Kamati hiyo alipofika mbele yake jana, jamii hizo mbili pia zinashikilia asilimia 41.5 kati ya nafasi 123 katika safu ya uongozi wa CBK. Kwa upande wake Mbunge wa Kisumu ya Kati Joshua Oron alielezea kukerwa na ripoti ya Dkt Thugge, iliyoonyesha kuwa jamii nne zinashikilia nafasi 800 kati ya 1,311 CBK.