Habari

Wabunge wataka Balala aadhibiwe kwa vifo vya vifaru 11

September 24th, 2019 3 min read

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Utalii na Wanyamapori Najib Balala huenda akaadhibiwa baada ya kamati ya bunge kupendekeza kuwa awajibikie vifo vya vifaru 11 weusi mwaka 2018 wakihamishwa kutoka mbuga za wanyama za Nairobi na Nakuru hadi ile ya Tsavo Mashariki.

Hata hivyo, adhabu hiyo itatolewa tu endapo kikao cha bunge lote kitaidhinisha pendekezo hilo la Kamati ya Bunge kuhusu Mazingira na Maliasili iliyowasilishwa bungeni Alhamisi wiki jana.

Pili, sharti Serikali Kuu ikubaliane na pendekezo hilo ndiposa Waziri Balala awajibikie kosa hilo kwa kuchunguzwa na asasi husika kwa lengo la kushtakiwa kwa kosa hilo.

Kamati hiyo ya Mazingira inayoongozwa na Mbunge wa Maara Kareke Mbiuki imekuwa ikichunguza uhamisho na vifo vya wanyama hao ambao ni idadi yao ni ndogo sana nchini.

“Kulikuwa na ulegevu kwa upande wa Wizara katika wajibu wake wa kusimamia utendakazi wa Shirika la Wanyamapori Nchini (KWS).” ripoti hiyo inasema.

Na inaongeza kuwa: “Kanuni na mwongozi ambao KWS hutumia katika shughuli ya kuwasafirisha wanyamapori nchini imepitwa na wakati.”

Kamati hiyo pia inasema kuwa uhamishaji wa wanyama hao hadi mbuga ya Tsavo Mashariki ulichochewa na ruzuku ya Sh2.8 bilioni ambazo Hazina ya Wanyamapori Dunia (World Wildlife Fund-WWF) ilipasa kupokea kutoka Ujerumani wala sio haja ya kulinda usalama wa wanyama hao.

Hazina ya WWF ndio ilifadhili shughuli hiyo ya kuwahamisha vifaru hao kutoka mbuga za Nairobi na Nakuru hadi ile ya Tsavo Mashariki.

Wabunge wanachama wa Kamati hiyo ya Mazingira na Mali Asili wanasema kuwa uhamisho huo ulilega nafasi kwa wafadhili hao kuona kwamba WWF “inawajali sana wanyama hao ili iweze kupata ufadhili kutoka Ujerumani”. Hii ni kinyume cha sera za kitaifa kuhusu uhifadhi wa wanayamapori.

“WWF ambayo ilikuwa inashirikiana na KWS katika uhifadhi wa vifaru ndio ilifadhili uhamisho huo lakini haikuwa na ruhusa kisheria kulishurutisha shirika la serikali (KWS) kukiuka kanuni na taratibu zilizowekwa katika shughuli hiyo,” ripoti hiyo inasema.

Uhamisho huo ulizinduliwa mwezi Juni mwaka jana kwa mbwembwe na Waziri Balala na wasimamizi wa WWF.

Vifaru hao walikuwa wakihamishwa hadi hifadhi mpya maalum katika Mbuga ya Kitaifa ya Tsavo Mashariki, hifadhi ambayo KWS na WWF ilijenga kwa kipindi cha miaka sita.

Shughuli hiyo ilikuwa imeratibiwa kuwa ya kila mara lakini vifo vya wanyama vilivyosababishwa na uwepo wa kiwango cha juu cha chumvi katika maji waliokunywa katika hifadhi hiyo mpya iliibua maswali kuhusu iwapo kweli Kenya imejitolea katika uhifadhi wa wanyamapori.

Tukio hilo pia ilikewa walimwengu, haswa wakereketwa wa uhifadhi wa wanyamapori haswa, wale ambao ni vivutio kwa watalii kama vile vifaru na ndovu.

Pia ilibaini kuwa Wizara Utalii na Wanyamapori na KWS zilipuuza hofu na malalamishi yaliyoibuliwa kuhusu hali ya afya ya wanyama katika hifadhi hiyo.

“Ni wazi kuwa haja kuwa wa wakuu wa wizara na KWS na WWF ilikuwa ni kujipatia fedha,” wabunge wanasema katika ripoti hiyo ambayo itakadiliwa bungeni wiki hii.

Kamati hiyo inayoongozwa na Bw Mbiuki pia inamlaumu Waziri Balala kwa kufeli kuteua Bodi Mpya wa Wakurugenzi katika KWS wakati huo, ambayo itatoa mwelekeo wa kisera na ushauri kwa wasimamizi wa KWS.

Ripoti hiyo inasema kuwa, kwa kuwa KWS haina Bodi ya Wakurugenzi wakati huo, wajibu wa kusimamia shughuli za KWS uko mikononi mwa Wizara ya Utalii na Wanyamapori.

Lakini baada ya vifo vya wanyama hao, Bw Balala aliteua wanachama wapya wa Bodi wa Wakurugenzi wa KWS.

Kamati hiyo inasema kuwa muda wa kuhudumu wa wanachama wa bodi ya zamani ulikamilika mnamo Aprili 17, 2018, “na miezi mitatu baada wanachama wa bodi mpya hawakuwa wameteuliwa, huku waziri akikosa kutoa sababu ya kutofanya hivyo.”

Katibu wa Wizara, ambaye alikuwa mwanachama wa bodi ya zamani, pia ameelekezea lawama na wabunge (katika ripoti hiyo) kwa kufeli kufeli kutoa usimamizi mwafaka wakati wa usafirishaji wa vifaru hao.

Wabunge hao pia wamependekeza kuwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) imchunguze mkuu wa usimamizi wa kitengo cha mazingira ya wanakoishi wanyamapori katika KWS kwa kudinda kutoa habari muhimu kuhusu ambayo ingezuia vifo hivyo.

Wabunge pia walisema haikujulikana ni kwa nini Wizara iliidhinisha uhamisho wa vifaru hao ilhali wanachama wa bodi ya zamani ya KWS waliwahi kuupinga mara tatu

Wanachama hao wa bodi waliamimu kuwa ilikuwa hatari kuwahamisha vifaru ambao wamezoea maisha huria mbugani hadi katika hifadhi yenye maji ili na kiwango cha juu cha chumvi kando na mazingira yasiyo mazuri kwa maisha ya wanyama hao.

“Wizara haikuonyesha kuwa imeshughulikia sababu kama hizo na kuondoa hatari kabla ya kuidhinisha uhamisho wa vifaru hao,” ripoti hiyo inasema.

Wabunge pia wanauliza ni kwa nini DCI haijamchunguza mkuu wa afya ya wanayamapori katika KWS, ambaye ndiye anasimami huduma za kuwakamata wanyama wanaohamishwa, kuhusiana na vifo vya vifaru wawili waliohamishwa kutoka Nakuru licha ya kwamba mmoja wao tayari alikuwa anaugua.