Habari

Wabunge watatu kutoka Magharibi wataka sheria ya TSC ifanyiwe marekebisho

September 28th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na SHABAN MAKOKHA na CHARLES WASONGA

WABUNGE watatu kutoka Kaunti ya Kakamega wamependekeza sheria ifanyiwe marekebisho kuhakikisha kuwa angalau mwalimu mmoja anateuliwa kuwa mwanachama wa Tume ya Kuajiri Walimu (TSC) ili kuwakilisha masilahi ya walimu.

Mbw Titus Khamala (Lurambi), Emmanuel Wangwe (Navakholo) na Johnson Naicca (Mumias Magharibi) walisema watashirikiana na wabunge wenzao kuhakikisha kuwa uanachama wa TSC unaakisi ule wa Tume ya Huduma za Bunge (PSC) na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC).

PSC na JSC zina wanachama wanaowakilisha wabunge na majaji, mtawalia.

Bw Khamala alilalamika kuwa muundo wa TSC sio sawa kwa sababu inakosa mwakilishi wa walimu.

Alisema sera nyingi zinazotungwa na TSC huishia kuwaumiza walimu kwa sababu hakuna anayewakilisha masilahi yao katika tume hiyo.

Bw Khamala alitoa mfano wa sera ya kuwahamisha walimu kama ambayo inaathiri utendakazi wao akisema familia za baada yao walimu hao zimevunjika kutokana na sera hiyo.

“Ikiwa walimu wataendelea kuathiriwa namna hii, basi bila shaka tunaharibu mustakabali wa watoto wetu. TSC imegeuka asasi ambayo haijali wala kushughulikia masilahi ya waajiri wake,” akasema Bw Khamala.

“Unaudhi kwamba ndoa change za walimu zinavunjika kutokana na sera kama hizi za uhamisho wa walimu bila kuzingatia mahitaji yao ya kimsingi,” akasema.

Na akiongea kwa simu Bw Wangwe alisema mswada huo wa marekebisho ya sheria ya TSC utawasilishwa katika bunge mwezi ujao wa Oktoba.

Bw Naicca pia anataka sheria ifanyiwe marekebisho ili masuala ya walimu yashughulikiwe na Maafisa wa Elimu katika ngazi ya Wilaya kwani wao ndio wanaelewa fika changamoto zinazowakabili walimu.

“TSC haielewi yale ambayo mwalimu wa kawaida, hasa yule anayeishi mashambani, anapitia maishani mwake. Hii ndiyo maana walimu kadha ambao ni wanachama wa Knut wameadhibiwa kuwa kupinga sera ya uhamisho wa walimu na utekelezaji wa mfumo mpya wa umilisi na utendaji (CBC),” akasema.

Kulingana na Bw Naicca, ikiwa walimu watajumuishwa kama wanachama wa TSC watakuwa katika nafasi nzuri ya kutetea masilahi yao.