HabariSiasa

Wabunge watisha kushtaki gazeti lililochapisha walipokea hongo ya Sh10,000

August 15th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

NA KALUME KAZUNGU

WABUNGE wawili wa Kaunti ya Lamu wametisha kulishtaki gazeti moja hapa nchini kwa kuchapisha majina yao kuwa miongoni mwa wabunge waliohongwa kwa Sh10,000 kila mmoja ili kutupilia mbali ripoti kuhusu sukari bandia hapa nchini.

Mbunge wa Lamu Mashariki, Athman Sharif na mwenzake wa Lamu Magharibi, Stanley Muthama, wanasema walioingiza majina yao kwenye kashfa ya sukari hapa nchini wako na lengo la kuwachafulia majina.

Wabunge hao wawili ambao wote wako nje ya nchi kwa shughuli za serikali, walilitaka gazeti la  Citizen Weekly lililochapisha majina yao Jumatatu kuomba msamaha mara moja la sivyo waelekee kortini.

Bw Sharif alikana kupokea mlungula wowote na kusisitiza kuwa kamwe hakuwa bungeni wakati ripoti kuhusu sukari bandia ilipowasilishwa bungeni na kamati ya Kilimo, Biashara na Uwekezaji mnamo Alhamisi wiki iliyopita.

“Mimi nilikuwa nimesafiri Mombasa Jumatano ili kuhudhuria uamuzi wa mahakama ya rufaa kuhusu uchaguzi wa gavana wetu wa Lamu, Fahim Twaha uliofanyika Alhamisi.

Sikuwa bungeni Nairobi na hakuna vile ningepokea rushwa inayodaiwa. Ninataka gazeti lililochapisha jina langu kuomba msamaha au niende kortini.

Kunihusisha na kashfa hiyo ni sawa na kuniua kisiasa. Pia ni kunivunjia heshima na kupaka matope jina langu. Sitakubali,” akasema Bw Sharif.

Naye Mbunge wa Lamu Magharibi, Stanley Muthama alitaja kashfa inayoendelea ya wabunge kuhongwa ili kuipuuza ripoti kuhusu uchunguzi wa sukari bandia kuwa propaganda.

Bw Muthama alisema hajui lolote kuhusu hongo inayodaiwa ilitolewa kwa wabunge ili kuikataa ripoti ya sukari.

Badala yake, Bw Muthama aliwataka viongozi kuelekeza fikra zao katika masuala yatakayonufaisha wananchi waliowachagua badala ya kujitahidi kuharibia wengine majina.

“Mimi niko nje ya nchi nikiwakilisha eneobunge langu katika masuala ya maendeleo. Yanayoenezwa nayachukulia kuwa propaganda tupu. Mimi sijapokea hongo kutoka kwa mtu yeyote na siwezi.

Fikra zao hasa zimejengwa katika kuhudumia wananchi wangu na kuhakikisha maeneo yanaafikiwa kwenye eneobunge langu na kaunti ya Lamu kwa jumla,” akasema Bw Muthama.