Wachezeana rafu
CHAGUZI ndogo zitakazofanyika wiki ijayo zimefungua uwanja wa vita vikali na majukwaa ya matusi huku mirengo ya serikali na upinzani ukiendelea kutifuana ikisaka ubabe na ushindi kwenye kura hiyo.
Migogoro ya ndani kwa ndani nayo imeshuhudiwa hasa miongoni mwa vyama tanzu kwenye Muungano wa Upinzani hasa katika kampeni za Malava na Wadi ya Kisa Mashariki kwenye Kaunti ya Kakamega.
Chaguzi ndogo zitakuwa zikiandaliwa maeneobunge ya Mbeere Kaskazini, Malava, Kasipul, Ugunja, Magarini pamoja na Useneta wa Baringo.
Kampeni za chaguzi ndogo za Ugunja, Magarini na Baringo hazijaonekana kushirikisha cheche kali ikilinganishwa na Mbeere Kaskazini, Kasipul na Malava.
Japo kuna chaguzi maeneo mengine ya udiwani, siasa kwenye wadi ya Kisa Mashariki zimefikia anga ya kitaifa kutokana na migogoro kati ya DAP na DCP.
Kilele cha matusi na lugha chafu kilidhihirika kwenye kampeni za aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua katika eneobunge la Mbeere Kaskazini mnamo Jumapili ambapo alitumia maneno makali kuwakashifu Rais William Ruto, Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku, Gavana wa Embu Cecily Mbarire na mwaniaji wa UDA Leo Muthende.
Bw Gachagua alidai kuwa Bi Mbarire alikuwa akipanga kuwasafirisha wageni kutoka, Nairobi, Kisii na Teso ambako ameolewa kushiriki uchaguzi huo mdogo.
“Tunataka kutangaza hapa kuwa siku ya kura hakuna mgeni atakubaliwa hapa Mbeere Kaskazini mpaka kura ipigwe na uchaguzi ukamilike,” akasema Bw Gachagua akishangiliwa na umati.
Kiongozi huyo wa DCP amekuwa na uhasama mkubwa na Bi Mbarire na wikendi gavana huyo alitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini imzuia Bw Gachagua kufanya kampeni Mbeere Kaskazini. Alidai kuwa DCP haina mwaniaji Mbeere Kaskazini na haikutia saini mwongozo wa uchaguzi.
Bw Gachagua pia alitumia lugha chafu isiyochapishika kuashiria kuwa iwapo Bw Muthende atashinda, Rais Ruto akisafiri kwa helikopta atapaa juu angani na kuwachekelea wakazi wa eneo hilo.
Kwa Bw Muthende mwenyewe, aliyekuwa naibu rais alidai kuwa si mpigakura wa eneo hilo na hawezi kuchaguliwa kuwakilisha watu wa eneo hilo.
“Huyo mvulana anatumiwa tu, hana shida na aliletwa tu hapa ambapo hata hapigi kura. Hata mke wake si mpigakura hapa, utampigiaje kura mtu ambaye hawezi kujichagua?” akauliza Bw Gachagua.
Kule Malava na Kisa Mashariki nao uhasama kati ya Gavana George Natembeya wa Trans Nzoia na Naibu Kiongozi wa DCP Cleophas Malala nao umefikia kilele chake.
Bw Malala alidai Gavana Natembeya ni fuko na DAP-K ilistahili kuachia DCP kiti cha Kisa Mashariki baada ya kuachiwa kile cha Malava.
Bw Natembeya amekuwa akiendesha kampeni zake maeneo hayo kivyake akiwa amevalia nguo zenye nembo ya vuguvugu lake la Tawe.
“Akirudi hapa siku nyingine, tutamtoa suruali uchi na nawaomba mpuuze huyo mtu. Ni tumbo mbele tu,” akasema Bw Malala akiwa kampeni wadi ya Kisa ambako alidai kuwa Bw Natembeya anadhaminiwa na serikali kusambaratisha upinzani.
Seneta wa Kakamega Bonny Khalwale na Naibu Gavana Ayub Savula nao wako sako kwa bako katika kumiminiana matusi kuhusu uchaguzi mdogo wa Malava.
Bw Khalwale anamuunga mkono mgombeaji wa DAP-Kenya Seth Panyako huku Bw Savula akirindima ngoma ya mwaniaji wa UDA David Ndakwa.
“Baada ya wabunge wote wa Kakamega kuniogopa na kunihepa sasa msaidizi wa Rais Farouk Kibet amenunua Savula aje anikabili. Nilienda Sports Club na kugundua kuwa pesa ambazo Savula amepewa kumbe ni kuandikiwa pombe kila jioni akishanitusi,” akasema Bw Khalwale kwenye kampeni.
Bw Savula naye alimjibu akisema kuwa anastahili kujisaili kwa sababu matusi yamemwezesha kutopiga hatua kisiasa ilhali aliingia bunge pamoja na Rais William Ruto 1997.
“Khalwale anatoka kwa akina mamangu na amekunywa chang’aa mpaka anasahau mamangu ni dadake. Huyo hana dira ya kuenda popote kisiasa,” akasema Bw Savula kwenye jukwaa moja na Bw Kibet.
Kasipul nayo kampeni imegeuka na kuishia damu kutokana na maafa watu wawili na wengine wakijeruhiwa katika matukio mbalimbali ya fujo.
Wafuasi wa mwaniaji wa ODM Boyd Were na mgombeaji huru Philip Aroko wamekuwa wakikabiliana wanasiasa hao wawili nao wakilaumiana.
Ghasia hizo zimesababisha chifu kufutwa kazi na maafisa wa Idara ya Upelelezi (DCI) kujeruhiwa wiki jana.