Wadau walalamika sekta ya maji inaingiliwa kisiasa
WADAU katika sekta ya maji wameelezea hofu kuhusu kile wanachotaja kama kuingizwa siasa katika usimamizi wa kampuni za maji nchini Kenya.
Walisema kuwa kuingiliwa kisiasa kwa shughuli za usambazaji maji kunahujumu usambazaji wa bidhaa hiyo kwa wateja.
Kulingana na Chama cha Wafanyakazi wa Kampuni za Huduma za Maji Nchini (WASWU) tatizo hilo linazuia kampuni hizo kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Akiongea Jumanne wakati wa kutiwa saini kwa makubaliano na Kampuni ya Maji na Usafi ya Embu (EWASCO), Katibu Mkuu wa WASWU Matilda Jebet alisisitiza kuwa japo kampuni za maji ziko chini ya serikali za kaunti, zimeundwa chini ya Sheria ya Maji na hivyo zinapewa uhuru kuendesha shughuli yazo.
Alisema kuwa kampuni hizo zinasimamiwa na wataalamu waliofuzu na ambao wanapaswa kuwa huru kufanya maamuzi kuhusu njia za kusimamia fedha fedha bila kuingiliwa na watu kutoka nje.
Jebet alieleza kuwa hatua ya wanasiasa kuingilia kampuni hizo kumedumaza ubunifu hali inayowazuia wahandisi na wataalamu wengine kutekeleza mapendekezo ya kupiga jeki kampuni wanazofanyia kazi.
Alisema kuwa katika baadhi ya kampuni, kampuni za maji zinasukumwa kurejea katika idara husika za kaunti, hatua ambayo alisema inaenda kinyume na Sheria ya Maji ya 2016 na ile ya 2023 inayotambua uhuru wa sekta ya maji.
Bi Jebet alionya kuwa hali ya sasa ambapo serikali haijawekeza katika miundo mbinu ya maji inaweza kusababisha changamoto katika sekta hiyo na kupelekea watu kupoteza nafasi za ajira.
Huku akitoa mfano wa mpango wa serikali wa kuunganisha stima hadi ngazi za vijijini, Katibu huyo Mkuu alisema serikali inafaa kuwekeza katika mpango sawa na huo katika sekta ya maji ili kuhakikisha kuwa bidhaa hiyo inawafikia wote.
Bi Jebet alilalamikia mishahara duni inayolipwa wataalamu katika sekta ya maji akisema iko chini ya viwango hitajika.
Alitoa mfano wa wahandisi waliohitimu kwa shahada ya diploma wanaolipwa mishahara ya Sh10,000 na akiitaka Bodi ya Kusimamia Huduma za Maji (WASREB) kuweka viwango vya mishahara vinavyooana na sera ya kitaifa ya maji.