Habari

Wafanyakazi wa NMG wachangia damu kusherehekea Sikukuu ya Wapendanao

Na MARY WANGARI February 13th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAFANYAKAZI wa kampuni ya Nation Media Group (NMG) Alhamisi walitoa damu kama ishara ya upendo na moja kati ya sehemu ya kuadhimisha sherehe za Sikukuu ya Wapendanao mwaka huu.

Kampeni hiyo yenye kaulimbiu “sambaza upendo” iliyofanyika katika jumba la Nation Center ilifanikishwa kupitia ushirikiano kati ya NMG na Huduma inayohusu Damu na Viungo vya Mwili Nchini (KBTTS).

Akitoa wito kwa Wakenya kujiunga na kampeni hiyo ya kutoa damu, Afisa Mkuu wa Utekelezaji (COO) NMG, Monicah Ndung’u, alisema shughuli hiyo ni ishara ya upendo inayodhamiriwa kuokoa maisha.

“Ulimwengu unapoadhimisha Sikukuu ya Upendo, tumechagua kupatiana kutoka moyoni – kwa uhalisia,” alisema Bi Ndung’u.

“Tunawahimiza raia kutoka nchini kote kujiunga nasi katika kampeni hii na kupitia hospitali au kituo cha kukusanyia damu cha KBTTS ili “kueneza upendo.”

Wafanyakazi wa Nation Media Group wakichanga damu kama mojawapo ya onyesho la upendo msimu huu wa Valentino. Picha|Billy Ogada

Ongezeko la visa vya maradhi sugu kama vile saratani, ugonjwa wa figo, anemia miongoni mwa watoto ikiwemo wahasiriwa wa ajali, ni miongoni mwa masuala ambayo yamesababisha haja ya damu kuongezeka kote nchini,” kulingana nan a Afisa wa Matibabu ya Maabara KBTTS, Eneo la Nairobi, Milka Omweri.

“Wakenya wasiopungua saba huhitaji kupatiwa damu kila baada ya sekunde 10 na wanakabiliwa na hatari ya kupoteza maisha yao ikiwa hakuna damu,” alieleza Bi Omweri.

Afisa huyo alifafanua kwamba Kenya haijatimiza viwango vinavyohitajika na Shirika la Afya Duniani (WHO) kuhusu damu inayotolewa kitaifa vinavyoagiza asilimia moja ya idadi ya watu nchini kutoa damu kila mwaka.

“Kenya tunahitaji 500 – 600 za damu inayotolewa kila mwaka kuambatana na masharti ya WHO,” alisema.

“Bado hatujafikia viwango hiv kama taifa. Mwaka uliopita, tulikuwa na 450,” alisema.

Kampeni ya kutoa damu ya KBTTS inayofanyika kila mwaka kilele chake kikiwa Sikukuu ya Wapendanao ilianza Jumatatu na itaendelea hadi mwisho wa Februari.

David Muthoka, ripota wa NTV alijawa na bashasha kwa kupata fursa ya kuchangia damu kwa mara yake ya kwanza.

“Nilijiambia ni sharti nifanye hivi. Hapo mbeleni sikuwahi kujishughulisha. Inachangia pakubwa kuokoa maisha. Sifanyi hivi kwa sababu yangu. Huenda siku moja nikahitaji kupatiwa damu,” alisema.

Kwa Maureen Kibunja kutoka Idara ya Mauzo, ilikuwa afueni kuu hatimaye kuweza kuchangia damu baada ya kujaribu mara kadhaa hapo awali bila kufua dafu.

“Nimekuwa nikitamani sana kutoa damu lakini hapo mbeleni sikuwa na damu ya kutosha. Nilijaribu nikiwa shule ya upili na chuo kikuu bila mafanikio. Nilikuwa na rafiki wa karibu ambaye mama yake alihitaji damu na nilihisi vibaya mno nilipofahamishwa siwezi kutoa damu.”

Wanaume wanaweza kutoa damu mara nne kwa mwaka kila baada ya miezi mitatu ilhali wanawake wanaweza kuchangia mara tatu kila mwaka kila baada ya miezi minne, anafafanua Bi Omweri.

Ili kutoa damu ni sharti uwe na umri kati ya miaka 15 – 65, una uzani wa kilo 50 kwenda juu, viwango vya damu 12.5 na zaidi na usiwe na matatizo ya kiafya.

Wanawake wajawazito, kina mama wanaonyonyesha, wanawake katika siku zao za hedhi na wagonjwa wanaougua maradhi sugu hawawezi kuchangia damu.