Habari

Wagonjwa hatarini madaktari katika kaunti tatu wakigoma

Na MERCY CHELANGAT  May 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KWA wiki kadhaa sasa, maelfu ya wagonjwa katika kaunti za Marsabit, Kakamega na Kiambu wameachwa bila huduma za matibabu baada ya zaidi ya madaktari 1,000 kugoma.

Akina mama waja wazito hawawezi kupata huduma ya kujifungua, watoto wengine matatizo sugu ya kiafya wanatelekezwa huku watu wazima wanaougua maradhi mbalimbali wakikosa tiba.

Katika kaunti ya Kakamega, wagonjwa wamekaa kwa wiki nne bila huduma baada ya madaktari kuamua kuendelea na mgomo.

Hali ilikuwa mbaya zaidi usiku wa kuamkia jana madaktari wa Marsabit waliamua kususia kazi huku jumla ya madaktari 324 walisitisha utoaji huduma hadi wakati usiojulikana.

Imekuwa vigumu kwa vituo vya afya kushughulikia hata wagonjwa wanaohitaji matibabu ya dharura.

“Imetulazimu kuwatuma wagonjwa wakahudumiwa katika hospitali za kibinafsi ambazo malipo yao ni ghali.

Aidha, tumekuwa tukiwaagiza kusaka huduma za afya katika kaunti za mbali ambazo tayari zimelewa na kazi,” akasema muuguzi mmoja katika hospitali iliyoathirika na mgomo na ambaye aliomba tulibane jina lake.

“Watu wanateseka, na wengine wanaishia kufanya kwa sababu hawawezi kupata huduma za matibabu wanazohitaji,” akasema Dkt James Maina Githinji, ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha Madaktari Nchini (KMPDU), tawi kati mwaka Kenya.

Madaktari hao wanataja kufeli kwa taratibu za ajira, ikiwemo kuhamishwa kwao kinyume cha sheria, kucheleweshwa kwa mishahara kila mara hali inayowalazimu kutumbukia kwenye madeni na kufanyakazi kwa muda mrefu.

“Hali kama hii imechangia baadhi ya madaktari kupatwa na matitizo ya kiakili, changamoto za kifedha, kupungua kwa moyo wa kufanyakazi, unywaji pombe kupindukia, kugura kazi na hata visa vya madaktari kujiua,” Dkt Githinji akasema.

Alisema KMPDU ilitoa ilani ya mgomo mnamo Mei 5 huku serikali za kaunti zikipewa kuwa wa siku 21 kushughulikia malalamishi ya wahudumu hao wa afya.

Serikali za kaunti zilifeli kabisa kushughulikia malalamishi ya madaktari licha ya barua kadhaa ziliwasilishwa kwao na chama cha KMPDU.

Huku madaktari wakipigania masilahi yao, ni wagonjwa wanaosaka huduma za afya ndio huumia zaidi.

“Katika kaunti ya Kiambu mishahara imekuwa ikichelewa kwa muda wa mwaka mmoja sasa. Kuna nyakati zingine ambapo mishahara huchelewa kwa hadi miezi miwili,” akaeleza Dkt Maina.

Rekodi za KMPDU zinaonyesha kuwa madaktari wa Kiambu walipokea mshahara wao wa Januari mnamo Februari 12 na mshahara wao wa Februari mnamo Machi 12, mshahara wao wa Machi wakiupokea Aprili 25 huku mshahabari wao wa Aprili ukiwafikia Mei 12.

“Pia tuna suala la uhamisho kiholela. Ijumaa kila wiki imekuwa wakati wa uhamisho. Hamna daktari aliye na uhakika mahala watafanyia kazi wiki itakayofuata. Hawa ni watu wenye familia. Katika familia kuna watoto wanaoenda shuleni. Kwa ukivurugwa na uhamisho wa kila mara ina maana kuwa masomo ya watoto wako pia yatavurugwa,” akasema Dkt Maina.