Wahadhiri wa chuo kikuu cha Moi waapa kurejea mgomoni wakishutumu ‘ahadi hewa’ za serikali
MGOGORO wa chuo kikuu cha Moi bado haujaisha huku Muungano wa Wahadhiri wa Vyuo Vikuu (UASU na vyama vya wafanyakazi wengine chuoni wakianza tena kususia kazi na kushutumu wasimamizi wa chuo hicho kwa kukosa kuheshimu mkataba wa kurejea kazini.
Wakizungumza na wanahabari mjini Eldoret Jumatatu, Januari 13, 2025, maafisa wa UASU waliapa kurejea barabarani mara moja huku wakidai mshahara wao wa Desemba.
“Tuliwasiliana na wasimamizi wa Chuo Kikuu cha Moi pamoja na maafisa wa wizara ambao walikubaliana kwamba wafanyakazi wa chuo kikuu cha Moi watalipwa mishahara yao ya Desemba leo la sivyo tunarudi mgomoni,” alisema Dkt Busolo Wegesa Katibu Mkuu UASU chuo cha Moi.
Dkt Busolo alishutumu chuo kikuu kwa mawasiliano duni ambayo yamechangia changamoto zinazokumba chuo hicho.
Hata hivyo, Dkt Busolo alisema kulipa mishahara ya mwezi Desemba kutafungua njia ya majadiliano zaidi ili kubaini sababu ya kwa nini chuo hicho kimeshindwa kutekeleza makubaliano kati ya uongozi na UASU kuhusu jinsi ya kuanza tena kazi katika chuo hicho.
“Tumezungumza na maafisa wa wizara ya elimu kuhusu jinsi ya kufanya kazi pamoja na usimamizi wa Chuo Kikuu cha Moi, na wakati wa majadiliano wizara ilikubali kuwa mishahara ya wafanyakazi wa chuo kikuu cha Moi itatolewa leo na mara tu tutakapolipwa hapo ndipo tutakapojua hatua inayofuata na jinsi ilivyo sasa hakuna kazi inayoendelea katika chuo hiki,” akasema Bw Wegesa.
Maoni yake yaliungwa mkono na katibu wa KUSU tawi la chuo hicho Mary Chepkwemoi aliyesema kuwa wafanyakazi wa chuo hicho wamepoteza imani na usimamizi kutokana na kushindwa kwa chuo hicho kutimiza ahadi za awali.
Bi Chepkwemoi alisema wafanyakazi wameapa kutorejea kazini hadi chuo kitekeleze vipengele vyote vya makubaliano ya kurejea kazini.
“Kutokana na kutokuwa na imani na usimamizi wa chuo kikuu tunarejea kugoma na haswa ikiwa mshahara wetu wa Desemba hautawekwa katika benki zetu na zaidi ni lazima chuo kitekeleze fomula ya kurejea kazini kwa jumla,” alisema Bi Chepkwemoi.
Mwishoni mwa mwezi Novemba 2024, wafanyakazi wa chuo hicho walisitisha mgomo ambao ulikuwa umedumu miezi mitatu baada ya kuafikia mwafaka na utawala wa chuo hicho.