Habari

Wahome audhi wanaokatwa ushuru wa nyumba: ‘Kukatwa ushuru haimaanishi kupata nyumba’

Na FRIDAH OKACHI February 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKENYA wameghadhabishwa na ufafanuzi wa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Miji, Bi Alice Wahome kuwa Ushuru wa nyumba nafuu hauwapi uhakika wa kumiliki nyumba chini ya mpango wa Boma Yangu.

Akizungumza Jumatano, kwenye mahojiano na NTV katika kipindi cha Fixing the Nation, Waziri huyo alisistiza kwamba ushuru huo si wa kuwekeza kupata nyumba zinazojengwa na serikali.

“Kuchangia Ushuru wa Nyumba hakuhakikishii mtu umiliki wa nyumba katika mpango wa Boma Yangu. Unachochangia si akiba, bali ni ushuru,” alisema Bi Wahome.

“Ushuru huo ni sawa na ushuru wa barabara. Unachangia hazina ya pamoja kumsaidia Mkenya mwingine kumiliki nyumba. Jukwaa hili ni la umma na ni wazi, hivyo kila mtu anaweza kupata nafasi ya kumiliki nyumba,” aliongeza.

Kwenye mtandao wa X, Wakenya walitaja ufafanuzi huo kuwa njia moja ya kuendeleza ufisadi.

“Kuanzisha ushuru wa kujenga nyumba za kuuzwa kwa walipa kodi lilikuwa wazo baya, na si ajabu mradi wa makazi nafuu umekosa kuafikia nyumba 200,000 kwa mwaka hadi chini ya 1,000. Hata wale wanaosimamia mradi huu hawawezi kueleza wazi manufaa yake,” alisema Antony Alexanderia Irungu.

“Kwa wakati ufaao, Wakenya wataelewa ni nani wanaonufaika na mpango huu wa makazi. Hawa si Wakenya,” aliongeza Sam Njuguna.

Uncommonson alisema: “Serikali hapo awali iliwasilisha ushuru wa makazi kama njia ya kutoa makazi nafuu, ikimaanisha kuwa wachangiaji wangenufaika moja kwa moja.”

“Maelezo gani ya kipuuzi haya? Mnatumia pesa zangu kujenga nyumba ambayo haitakuwa yangu hadi ninunue,” alisema Linda Oriedo.

Wakati huo huo, Bi Wahome alihakikishia umma kuwa serikali inajitolea kuhakikisha uwajibikaji katika mpango huu ili Wakenya wengi iwezekanavyo, hasa wale wa kipato cha chini waliolengwa, waweze kupata makazi bora.

Alisema malipo hayo ya nyumba nafuu, yanalenga kuwezesha umiliki wa nyumba kupitia mfumo wa ‘lipia na umiliki’, ambapo wanaonufaika hulipa kiasi fulani kila mwezi kwa muda wa miaka 30.

“Kwa Sh3,900 pekee kwa mwezi, mtu anaweza kumiliki nyumba. Hakuna anayehitajika kulipa Sh640,000 moja kwa moja. Kiasi hiki kimesambazwa kwa miaka 30, hivyo kumiliki nyumba kunakuwa rahisi zaidi,” alieleza.

Waziri Wahome alitangaza kuwa serikali itatoa nyumba 4,888 kufikia mwisho wa Machi 2025. Aidha, kati ya nyumba 4,000 hadi 5,000 zitakuwa zikitolewa kila robo mwaka.