Habari

Wahudumu waliookoa maisha wakati wa corona walilia malipo afisini kwa Duale

Na LEON LIDIGU May 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ZAIDI ya wahudumu wa afya 8,500 walioajiriwa kwa mkataba chini ya mpango wa Huduma ya Afya kwa Wote (UHC) waliandamana barabarani kushinikiza waajiriwe kazi ya kudumu na ya pensheni pamoja na kulipwa marupurupu ambayo wamekuwa wakiahidiwa kwa muda mrefu.

Wakibeba mabango na kuimba, waandamanaji wanataka kulipwa mishahara kamili kulingana na viwango vya sasa kama ilivyowekwa na Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC) na kuidhinishwa kwa bajeti ya kuwalipa kabla ya kuhamishiwa serikali za kaunti.

Wahudumu hao wa afya, waliokuwa mstari wa mbele kukabiliana na janga la Covid-19 mwaka 2020, walisema wameachwa bila mwelekeo kwa miaka mitano, wakifanya kazi kwa mikataba isiyobadilika, wakilipwa mshahara wa chini kuliko wenzao na sasa wanakabidhiwa kaunti bila mipango sahihi ya mpito au ulinzi wa kifedha.

“Tuko hapa kuandamana kwa sababu tumeonewa. Tunataka marupurupu yetu yalipwe kwa sababu tumefanya kazi kwa miaka mitano bila chochote cha kuonyesha. Tumempoteza mwenzetu katika ajali ya barabarani alipokuwa akisafiri kutoka Taita Taveta kuja kushiriki maandamano. Alikufa akipigania haki yake ya kulipwa vizuri,” alisema Doris Ndui, mhudumu wa UHC kutoka Kaunti ya Meru.

Tangu kuanzishwa kwa mpango wa UHC, wahudumu hao walisema wamewapoteza wenzao 44, wengi wao kwa kujiua.

“Tunabeba mzigo mzito wa kihisia. Mishahara yetu ni robo ya wale wanaofanya kazi sawa. Serikali ilitutumia halafu ikatutupa,” alisema Bi Ndui, aliyekuwa ameshika bango lililoandikwa “waliotuacha”, likiwa na majina ya wenzake waliopoteza maisha.

Wahudumu hao walimkosoa Waziri wa Afya Aden Duale, wakisema alikimbilia vyombo vya habari kusema wamekubali kufanya kazi katika mazingira hayo duni ilhali hakuna makubaliano yoyote rasmi yaliyosainiwa kuhusu kurejea kazini.

Jumanne wiki iliyopita, katika kikao kilichoongozwa na Waziri Duale pamoja na Baraza la Magavana (CoG) na vyama vya wafanyakazi wa sekta ya afya wakiwemo Katibu Mkuu wa Chama cha Wauguzi (KNUN) Seth Panyako, ilitangazwa kuwa kuanzia Julai 1, 2025, usimamizi wa  mishahara ya wahudumu  wa afya wa UHC utahamishiwa serikali za kaunti pamoja na bajeti inayohitajika kuendeleza masharti ya sasa wakati wa mpito.

“Kabla ya mikataba ya sasa kumalizika, serikali za kaunti zitapokea fedha za nyongeza kuwezesha kuajiri wafanyakazi wa UHC kwa masharti ya kudumu. Vilevile, malipo ya marupurupu yatazingatiwa baada ya mchakato wa kuwaajiri kudumu,” alisema  Duale.

Hata hivyo, akizungumza na Taifa Leo pembezoni mwa maandamano hayo, Mwenyekiti wa Kitaifa wa Wafanyakazi wa UHC, Desmond Wafula, alisema hawakualikwa katika mkutano huo bali wizara iliamua ‘kufikia makubaliano’ na Bw Panyako ambaye hawawakilishi.

“Alichokubaliana Bw Panyako na Duale hakina msingi wowote nasi tunakikataa kwa sababu hatukuhusishwa wakati masuala yetu yalikuwa yakijadiliwa na kuidhinishwa,” alisema Bw Wafula.

“Hatuondoki Afya House leo. Kwa kweli, hatujui lini hasa tutaondoka. Kuanzia leo usiku tutaandaa maombi ya usiku hadi yale tuliyoahidiwa yatimizwe na haki zetu ziheshimiwe,” aliongeza Bw Wafula