Waiganjo amtetea Gachagua anapokabiliwa na hoja ya kutimuliwa
MFANYABIASHARA Joshua Karianjahi Waiganjo, aliyeachiliwa na mahakama kuu katika kesi za kujifanya afisa mkuu wa polisi Ijumaa, alijitokeza kufafanua kwamba mojawapo ya kampuni zilizotajwa bungeni katika mswada wa kumtimua mamlakani Naibu Rais Rigathi Gachagua ni yake.
Kampuni hii inayoajulikana kwa jina Morani Manufacturers Limited ina wakurugenzi watatu mmoja wao akiwa ni mkewe Bw Gachagua, Pasta Dorcus Rigathi pamoja mwana wao Keith Ikinu Rigathi.
Bw Waiganjo amekana kampuni hiyo ilipokea Sh5.2 bilioni kutoka kwa serikali kama ilivyodaiwa bungeni na Mbunge wa Kibwezi West Mwengi Mutuse.
Bw Waiganjo aliyepata umaarufu kwa kutembea na wakuu wa polisi kwa kuvaa sare za polisi alisema kampuni ya Morani Manufacturers Limited ni yake na wala sio ya Bw Gachagua.
Katika taarifa aliyowasilisha katika Mahakama kuu na Bungeni Ijumaa Oktoba 4,2024 Bw Waiganjo amefafanua aliandikisha kampuni hiyo Oktoba 13,2021.
Kupitia kwa mawakili Sam Nyamberi, Danstan Omari na Shadrack Wambui, Bw Waiganjo amesema tangu aisajili kampuni hiyo ameuza tu mara moja chakula cha nguruwe cha Sh132,000.
“Ijapokuwa niliwauzia Dorcus Wanjiku Rigathi (mkewe Naibu Rais Rigathi Gachagua), Keith Ikiru Rigathi hisa kampuni hii haijawahi pokea Sh5.2bilioni zilizodaiwa bungeni na Mbunge wa Kibwezi West Mwengi Mutuse aliyewasilisha mswada wa kumtimua ofisini Naibu Rais Jumanne (Oktoba 1,2024),” Bw Waiganjo amesema katika taarifa kwa mahakama na bunge.
Bw Waiganjo amefafanua kuwa aliwauzia hisa 200 kila mmoja mkewe Gachagua na mtoto wake.
Katika hati ya kiapo aliyowasilisha bungeni, Bw Waiganjo anaomba jina la kampuni hiyo itolewe katika orodha ya kampuni anayodaiwa kumiliki Bw Gachagua.
Bw Waiganjo ameeleza pia ataomba majina ya mkewe Gachagua na mwanao yaondolewe katika mashtaka ya kumtimua kazini Naibu Rais.