Waiguru sasa atangaza arusi rasmi
Na BENSON MATHEKA
HATIMAYE Gavana wa Kirinyaga Anne Mumbi Waiguru na mchumba wake wakili Kamotho Waiganjo, wametangaza rasmi arusi yao baada ya sherehe ya posa iliyokuwa ya kibinafsi.
Wawili hao wamealika marafiki katika shule ya msingi ya Kiamugumo, Kirinyaga ambako watafanyia arusi ya kitamaduni mnamo Julai 13, 2019.
Mnamo Februari 26, wawili hao waliandaa sherehe ya kitamaduni ya posa lakini kwa kutoa mwaliko kwa marafiki, arusi yao inatarajiwa kuhudhuriwa na watu mashuhuri nchini wakiwemo wanasiasa.
Kulingana na desturi ya jamii za Agikuyu, sherehe watakayoandaa Julai inafahamika kama ngurario ambapo jamaa wa pande zote hukutana kushuhudia awamu ya mwisho ya ndoa ya kitamaduni na kumsindikiza bi harusi kwa boma la mumewe.
Katika sherehe hiyo, Bw Waiganjo anatarajiwa kumtambua mchumba wake kutoka wa kundi la wanawake watakaovalishwa mavazi yanayofanana.
Na baada ya kukamilisha sherehe hiyo, wawili hao watakabidhiwa cheti cha ndoa.
Mahari yatolewa
Mnamo Februari 16 Bw Kamotho alilipa mahari kumuoa Bi Waiguru katika hafla iliyofanyika kijiji cha Kiamungo, kaunti ya Kirinyaga.
Walioshuhudia hafla hiyo walisema alikuwa amevalia mavazi ya asili ya Kiafrika.
Picha za sherehe hiyo zilipenya katika mitandao ya kijamii na vilevile tovuti mbalimbali zinazoangazia masuala ya wapenzi na wachumba.