Waititu apata afueni, aagizwa alete dhamana ya Sh53 milioni atoke jela
JAJI wa Mahakama Kuu, Lucy Njuguna, amepitia upya agizo lake la awali na kukataa ombi la Ferdinand Waititu la kuachiliwa kwa dhamana akisubiri uamuzi wa rufaa yake.
Badala yake, aliamuru kuwa Waititu apate “dhamana ya benki inayokubalika” kulipa faini yote aliyotozwa baada ya kupatikana na hatia ya ufisadi.
Mahakama ilibainisha kuwa Waititu alikuwa ameomba kuachiliwa kwa misingi ya hali yake ya kiafya inayozidi kudorora, pamoja na mzigo anaosababishia Huduma ya Magereza nchini kutokana na kulazwa kwake katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH).
“Mahakama hii haina sababu wala ushahidi mwingine kutoka kwa upande wa mashtaka unaoweza kupinga ripoti ya kiafya iliyo mbele ya mahakama kuhusu hali ya mlalamishi. Kwa mahakama hii, haya ni mazingira mapya yanayohalalisha mahakama kutumia mamlaka yake na kupitia upya uamuzi uliotolewa Machi 3, 2025,” alisema Jaji Njuguna.
Aliyekuwa Gavana wa Kaunti ya Kiambu alipatikana na hatia Februari 14 na kuhukumiwa kifungo cha miaka 12 gerezani au kulipa faini mbadala ya Sh53 milioni.
Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Ufisadi, Thomas Nzyoki, alipata Waititu na hatia ya kushiriki katika vitendo vya ufisadi alipokuwa gavana wa Kiambu.
Mahakama ilibaini kuwa Waititu alipokea Sh 25 milioni kutoka kwa kampuni ya Enterprise Testimony Ltd, ambayo ilikuwa imepatiwa zabuni ya barabara ya Sh588 milioni na serikali ya kaunti ya Kiambu.
Fedha hizo alipokea kupitia kampuni zake mbili, huku akijua wazi kuwa zilikuwa mapato ya uhalifu.
Maombi yake ya awali ya kuachiliwa kwa dhamana yalikataliwa mara mbili. Aliwasilisha ombi la tatu akiomba mahakama ipitie upya uamuzi wake, akieleza kuwa alikimbizwa KNH Mei 13 baada ya hali yake ya kiafya kuzorota zaidi.
Kupitia kwa mawakili wake, John Swaka na Kibe Mungai, Waititu alieleza kuwa maisha yake yako hatarini na kwamba Gereza la Kamiti au gereza lolote nchini halina uwezo wa kushughulikia hali yake.
Mawakili wake walisema Waititu anasumbuliwa na kisukari, shinikizo la damu, matatizo ya macho na figo pamoja na kufanyiwa upasuaji mara kadhaa.
Wakili Swaka aliongeza kuwa rufaa aliyowasilisha ina mashiko na nafasi kubwa ya kufanikiwa kwa kuwa upande wa mashtaka haukuwasilisha ushahidi unaoonyesha kuwa serikali ya Kaunti ya Kiambu ilipoteza pesa zozote.
Alisema kesi hiyo iliendeshwa kwa misingi ya dhana potofu za umma na maoni ya kisiasa yaliyojaa chuki dhidi yake. Aidha, alisisitiza kuwa wakati wa kesi, alitii masharti yote ya mahakama na hakuwa na nia ya kutoroka.
Upande wa mashtaka ulipinga kuachiliwa kwake kwa dhamana, ukisema kuwa hakuna rekodi za matibabu zinazoonyesha kuwa hali yake ni mbaya kama anavyodai.
Mahakama pia ilielezwa kuwa Waititu alifanyiwa uchunguzi wa kitabibu akiwa Kamiti, na ripoti kamili ya afya yake ikawasilishwa mahakamani ikithibitisha kuwa anapata matibabu anavyohitaji.