Habari

Waititu ataka mahakama impunguzie masharti ya dhamana arudi ofisini

July 31st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

GAVANA wa Kiambu, Ferdinand Waititu Baba Yao amewasilisha ombi katika Mahakama Kuu, akitaka apunguziwe masharti ya dhamana aliyopatiwa Jumanne baada ya kushtakiwa kwa ufisadi akisema ni kubwa na inakiuka Katiba.

Hakimu Lawrence Mugambi alimwagiza Bw Waititu na washtakiwe wengine Zacharia Njenga Mbugua na Bi Joyce Ngina Musyoka kulipa Sh15 milioni pesa taslimu au waweke dhamana ya Sh30 milioni kila mmoja.

Hakimu alimwachilia mke wa Bw Waititu, Susan Wangari kwa dhamana ya Sh4 milioni na washtakiwa wengine wakaachiliwa kwa dhamana ya Sh1 milioni.

Washtakiwa wote walilala rumande ingawa baadhi yao walilipa dhamana lakini hawakuweza kuachiliwa kwa kukosa kukamilisha utaratibu unaofaa.

Kwenye ombi lake katika Mahakama Kuu, Bw Waititu anakosoa uamuzi wa Hakimu Mugambi akisema kiwango alichoagizwa kulipa ni sawa na kumnyima dhamana.

Masharti makali

Kupitia wakili wake Tom Ojienda, Gavana huyo anasema kwamba mahakama ilimwekea masharti makali ilhali hakukuwa na sababu za kutosha kufanya hivyo.

Bw Waititu anakosoa agizo la kumzuia kuingia katika ofisi yake akisema ni sawa na kumvua wadhifa wa ugavana.

“Masharti haya ni ya kumuondoa ofisini kinyume cha sheria,” anasema.

Kwenye ombi lake, Bw Waititu anasema kulingana na sheria, mtu anayeshikilia wadhifa wa kikatiba, hawezi kusimamishwa kazi bila kufuatia utaratibu uliowekwa kisheria wa kumuondoa.

Ingawa mahakama ilisema naibu gavana anaweza kutekeleza majukumu ya gavana aliyesimamishwa kazi, Bw Waititu anasema sheria imeweka mipaka ya majukumu ya naibu gavana.

“Sheria ya serikali ya kaunti inafafanua kwamba majukumu ya naibu gavana ni yale anayoapatiwa na gavana,” anasema.

Anataka mahakama kukubaliana naye kwamba dhamana hiyo ni kubwa na kuipunguza kwa sababu inazidi kiwango cha pesa ambazo gavana huyo na washtakiwa wenzake wanadaiwa kupora.

Gavana huyo anataka Mahakama kuu ifafanue hatua ya kumzuia kuingia katika ofisi yake na athari za agizo hilo kwa wakazi wa Kaunti ya Kiambu.

Kulingana naye, kukatazwa kuingia katika ofisi yake ni kukiuka haki za kisiasa za wakazi wa kaunti ya Kiambu.

Aidha, anataka mahakama ieleze ikiwa hakimu alikosea kwa kutumia uamuzi wa kesi ya Gavana wa Samburu Moses Kassaine kumzuia kuingia katika ofisi yake.