Wakazi Baringo waomboleza Mzee Moi kwa maandamano
FLORA KOECH Na WYCLIFFE KIPSANG
WAKAZI wa Kaunti ya Baringo waliomboleza hayati Daniel Moi kwa maandamano na kufunga barabara ya Kabarnet – Kabartonjo wakilalamikia kutengwa na serikali zilizofuata utawala wake.
Serikali hizo ni za Rais Mstaafu Mwai Kibaki na ya sasa inayoongozwa na Uhuru Kenyatta.
Huku wakiimba nyimbo za kumsifu Mzee Moi, wakazi hao walilalamika kuwa serikali zilizokuja baada ya utawala wa miaka 24 ya Mzee Moi zilipuuza Kaunti ya Baringo baada yake kustaafu 2002.
Walisema kuwa Naibu Rais William Ruto alizuru eneo hilo miaka miwili iliyopita na kuahidi kuwa serikali imetenga Sh300 milioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo lakini kufikia sasa ingali mbovu.
“Hatukutaka kuandamana wakati huu ambapo tumepoteza kiongozi wetu. Lakini hiyo ndiyo njia ya pekee ya kuelezea masaibu yetu,” akasema Stanley Kipkechem, mkazi.
Wakazi hao walisema barabara hiyo ya kilomita 30 inayounganisha Kabarnet, Kabartonjo na Kipsaraman ilijengwa na Mzee Moi miaka 40 iliyopita na haijawahi kufanyiwa ukarabati tangu alipostaafu.
“Mzee Moi alifanyia Kenya mambo mengi na ni aibu kwamba miradi aliyoanzisha imepuuzwa na serikali baada yake kustaafu,” akasema Evans Sengech.
Shughuli za usafiri zilitatizika kwa saa kadhaa baada ya waandamanaji hao kufunga barabara hiyo kwa kutumia mawe na matawi ya miti.
Polisi walilazimika kuingilia kati kuondoa vizuizi hivyo.
Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo ulibaini kuwa miradi mingi iliyoanzishwa na serikali ya Mzee Moi ilikwama baada ya kustaafu.
Miongoni mwa miradi hiyo ni Shirika la Kufadhili Wakulima (AFC) na Chama cha Wakulima (KFA).
Shughuli katika Hoteli ya Kabarnet ambapo Mzee Moi alikuwa akivinjari mara kwa mara akiwa na maafisa wengine wakuu serikalini zimepungua kwa kiasi kikubwa.
“Tangu Moi alipokuwa mbunge wetu na kisha akawa rais, eneo la Baringo halikuwahi kukumbwa na njaa. Tangu astaafu njaa imekuwa kawaida Baringo. Tumepoteza nguzo muhimu,” akasema Ronald Komen, mkazi wa kijiji cha Salawa.