Habari

Wakazi Mombasa wakosa maji safi

June 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MISHI GONGO

MAENEO mengi mjini Mombasa yanaendelea kukosa maji safi ya kunywa huku wakazi wakitaka kampuni ya kusambaza maji mjini humu (Mowasco) kutatua shida hiyo kwa haraka.

Wakazi wengi wamekuwa wakilalamika kuwa mitaa wanayoishi inakosa maji, jambo hivyo kulazimika kununua bidhaa hiyo muhimu kwa wachuuzi.

Mitaa iliyoathirika kutokana na ukosefu huo ni Changamwe, Kisauni, Bamburi, na Kiembeni.

Kulingana na wakazi uhaba huo umepelekea wakazi kutozwa ada za juu kununua maji.

“Kawaida mtungi mkubwa wa maji ni Sh20 lakini sasa hivi tunaununua kwa Sh50 hali inayofanya sisi tulio na familia kubwa kuumia kwa sababu twalazimika kununua mitungi zaidi ya 10,” akasema Bi Mary Wairimu mkazi wa V.O.K.

Mwengine Bw Juma Hassan kutoka Bamburi alieleza kuwa hali hiyo inawapa wasiwasi kwani wanashindwa kutekeleza masharti yaliyowekwa na Wizara ya Afya kupambana na virusi vya corona.

Alisema uhaba wa maji unawazuia kuosha mikono mara kwa mara kama inavyotakiwa.

“Maji tunayopata ni kidogo hivyo tunashindwa kuosha mikono mara kwa mara,” akasema.

Kulingana na mkurugenzi katika shirika hilo Bw Anthony Njaramba, uhaba huo unatokana na kukauka kwa bwawa la Marere na Mzima kufuatia jua kali linaloendelea kushuhudiwa Pwani.

“Mabwawa haya ni ya misimu. Hakuna maji kwa sababu yamekauka. Hata hivyo, tunafanya juhudi wakazi wapate maji,” akasema.

Bw Njaramba amesema wamekuwa wakisambaza lita 30,000 kila siku na kiwango hicho kinatosheleza wakazi wote wa Mombasa.