Habari

Wakazi Thika waitaka Nema imakinike kuboresha mazingira

August 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Thika wanaitaka Halmashauri ya Kutunza Mazingira (Nema) ichukue jukumu kuona ya kwamba mazingira yanahifadhiwa inavyostahili.

Wakazi wa Umoja na Matharau, mjini Thika, wamewasilisha malalamiko yao kwa mbunge wao Bw Patrick Wainaina, wakimtaka aingilie kati kutatua shida yao.

Bw Wainaina ameitaka Kaunti ya Kiambu kuchukulia jambo hilo kwa uzito unaostahili kwa kujadiliana na Nema ili kupata suluhisho.

Alisema Alhamisi kwamba viwanda vingi vimekuwa vikiacha majitaka kuingia katika mito miwili muhimu ya Komo na Ndarugo na hiyo imesababisha wakazi wengi kutumia maji machafu yanayosababisha maradhi mengi mwilini.

“Tayari nimezungumza na Kaunti ya Kiambu kuingilia kati kwa kuwasiliana na Nema ili kujua ukweli wa mambo uko wapi. Tayari wakazi wengi wameathirika kutokana na maji hayo machafu,” alisema Bw Wainaina.

Alisema iwapo hakuna jambo la maana litafanyika, bila shaka hatua ya kisheria inastahili ili kuwaokoa wakazi hao wasije wakaathirika zaidi.

“Ni mara kadha wakazi hao wenyewe wamelalamika kupitia Nema, lakini hakuna lolote limefanyika kuwaokoa. Kwa hivyo, mimi mbunge wa eneo hili ninaona ni vyema kuchukua hatua zaidi,” alisema mbunge huyo.

Alisema atalazimika kufanya kikao na wakuu wa Kaunti ya Kiambu na wale wa Nema ili kujua ukweli wa mambo uko wapi.

Hatua kuchukuliwa

Aliyasema hayo alipofanya mkutano na wakazi wa Thika waliotoa malalamiko yao kwake wakitaka hatua ichukuliwe haraka iwezekanavyo.

“Sisi kama wakazi wa Umoja tumetaabika vya kutosha kwa sababu kuna viwanda kadha katika eneo la viwandani vinavyoharibu mazingira kwa kumwaga uchafu wote unaotoka katika maeneo yao hadi katika mito tunayotumia kwa mahitaji yetu ya kiafya,” alisema Bw Joseph Munyao.

Alisema wakazi wengi wameambukizwa maradhi tofauti ya kifua, ngozi, na homa ya matumbo kutokana na matumizi ya maji machafu yanayomwagwa mabaki yote kutoka viwandani, na kuongeza hata wengine wameathirika hata macho.

Alisema hakuna mkazi yeyote aliye na usalama wa kiafya na wengi wao wanaishi katika maisha ya kubambanya bila kujua utakula nini siku inayofuata.