Habari

Wakazi wa mtaa wa Langas, Eldoret wang’ang’ania Krismasi ya mapema

Na TITUS OMINDE December 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KRISMASI ya mapema kwa wanawake kutoka mtaa wa mabanda wa Langas iliyotolewa na mfanyabiashara mmoja wa eneo hilo nusra iwe karaha pale walengwa walipoanza kung’ang’ania chakula hicho.

Ilibidi maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Langas kuingilia kati ili kurejesha utulivu na kutoa nafasi kwa mhisani kugawa chakula hicho katika mazingira tulivu.

Chakula hicho kilitolewa na mfanyabiashara Florence Akinyi.

Bi Akinyi alifanikiwa kulisha watu wapatao 2,000 huku akitoa wito kwa wahisani wengine kujitokeza na kuwafaa wakazi hao.

“Idadi kubwa ya watu ambao wamejitokeza hapa ni ishara ya umaskini katika mtaa huu, kuna haja ya wadau zaidi kujitoekeza angalau kuwasaidia siyo tu wakati wa Krismasi bali mara kwa mara,” alisema Bi Akinyi maarufu Mama Dota.

Hata hivyo, Akinyi aliwataka wenyeji kujisajili katika mipango ya serikali ya kuwafaa wananchi wa matabaka ya chini kama vile miradi inayolenga akina mama mboga, walemavu miongoni mwa miradi mingine.

“Kama mwenyeji ambaye naelewa hali ya maisha katika kijiji hiki niliamua kuwapa Krismasi ya mapema, nililenga watu 2,000 lakini kuna watu wengi ambao wanahitaji msaada kama huu mtaani humu,” alisema Bi Akinyi.

Baadhi ya akina mama walionufaika walisifia Bi Akinyi kwa msaada huo wakisema kuna haja ya serikali kuwezesha wenyeji ili wawe wakijimudu maishani.

“Huyu mama amefanya jambo nzuri zaidi, maisha katika mtaa huu ni magumu sana, nataraji huu ndio mwanzo wa misaada zaidi,” alisema Susan Mmbone ambaye ni mmoja wa watu walionufaika.

Msaada huo ulikuwa ni unga wa ngano, chumvi, sukari, mchele miongoni mwa vyakula vingine.