Habari

Wakazi wakimbilia vichakani visa vya utovu wa usalama Kitui Kusini vikizidi

Na BONIFACE MWANIKI August 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKAZI wa eneo la Musenge katika wadi ya Mutha, Kitui Kusini wanalazimika kulala vichakani usiku kufuatia visa vya mara kwa mara vya ukosefu wa usalama ambavyo vimewalazimu kutoroka makwao.

Katika tukio la hivi punde, wakazi walichomewa nyumba zao na watu wanaoshukiwa kuwa wachungaji mifugo wenye asili ya Kisomali.

Kulingana na waathiriwa ambao sasa wanaishi kwenye vibanda vya muda karibu na soko la Musenge, baada ya nyumba zao kuchomwa, visa vya ukosefu wa usalama vimekuwa vya kawaida eneo hilo kwa zaidi ya miaka 30 sasa.

Kamene Nzumbi, mkazi wa eneo hilo aliambia Taifa Leo kwamba nyumba zake nne zilichomwa na majangili, jambo lililomlazimu yeye, wanawe wa kiume pamoja na wake wao wanne – watatu wao wakiwa wajawazito kutoroka.

“Walivamia shamba langu na makundi ya ngamia. Nilipojaribu kuwakemea walifyatua risasi hewani mara kadhaa, nikalazimika kukimbia. Baadaye, walichoma nyumba zetu zote. Vitu vyetu vyote vya nyumbani na mavazi viliungua na sasa tumebaki bila makazi,” alisimulia Kamene.

Kamene sasa anatoa wito kwa serikali kuingilia kati kwa dharura, ikiwezekana kuwapa chakula na mavazi kwanza kabla ya kurejesha usalama eneo hilo.

“Tunaomba msaada wa dharura kutoka kwa serikali kurejesha amani katika eneo letu, lakini kwa sasa tunahitaji msaada wa chakula na mavazi ili tuweze kuendelea kuishi,” aliongeza.

Bw Jackson Muli, mwathiriwa mwingine, anashangaa ni muda gani serikali itachukua kuwapa wakazi wa eneo hilo amani ya kudumu, kwani kutoroka makwao kila mara kumegeuka kuwa jambo la kawaida.

Hata shule ya karibu ya msingi ya Musenge imeathirika, huku idadi ya wanafunzi ikishuka sana wakati shule zinafunguliwa kwa muhula wa tatu.

Wasichana wadogo wanakimbilia ndoa za mapema, wengine wakikosa hata mahitaji ya kimsingi na sare za shule.

Kulingana na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Musenge, Bi Eunice Kamende, shule hiyo imekuwa ikipambana kutoa elimu kwa wanafunzi kutokana na hali ya ukosefu wa usalama, ambapo walimu wengi wameamua kukaa nyumbani hadi usalama utakaporejeshwa.

Seneta wa Kitui, Bw Enoch Wambua, wiki iliyopita alielezea wasiwasi wake kuhusu jinsi utawala wa eneo hilo chini ya Wizara ya Usalama wa Ndani unavyoshughulikia suala hilo, akidai kuwa wameshindwa na kumtaka Rais William Ruto kuingilia kati.