Habari

Wakenya 15 hatarini kufurushwa Amerika

Na BENSON MATHEKA December 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SERIKALI ya Amerika imetangaza kuwa itawafurusha Wakenya 15 miongoni mwa maelfu ya raia wa kigeni ambao wamehukumiwa kwa makosa mbalimbali kutoka nchi hiyo.

Haya yanajiri katikati ya msururu wa misako ambayo serikali ya Rais Donald Trump inataja kama hatua ya kuwaondoa “wageni wabaya.”

Kundi hilo ni miongoni mwa wahalifu walio katika orodha iliyotayarishwa na Wizara ya Usalama wa Ndani ya Amerika kuhusu wahamiaji wasio na stakabadhi waliokamatwa kwenye misako hiyo.

Orodha hiyo inajulikana kama ya ‘wabaya kuliko wote’ na inachukuliwa kama hatua mpya ya kuiwezesha serikali ya Trump kutangaza hadharani visa vya kukamatwa kwa wahamiaji na kuongeza uwazi kuhusu mpango wake wa kuwafurusha.

Wakenya 15 waliotajwa kwenye orodha hiyo ni Alfred Obiero mkazi wa Colorado Springs, aliyehukumiwa kwa kushambulia, kuendesha gari akiwa mlevi, na dhuluma za nyumbani, Bethuel Gathu anayeishi Chowchilla, California ambaye alihukumiwa kwa wizi wa kutumia nguvu, Patrick Mwangi (San Antonio, Texas) aliyehukumiwa kwa kuendesha gari akiwa mlevi na Daniel Kathii mkazi wa Conroe, Texas ambaye alihukumiwa kwa kuendesha gari akiwa mlevi.

Wengine ni Mohamed Chekchekani wa San Pedro, California ambaye makosa yake ni kumteka mtoto na kukiuka Sheria kuhusu makundi ya uhalifu, Moffat Muriithi wa mji wa Seguin, Texas aliyehukumiwa kwa makosa yanayohusiana na dawa za kulevya, Francis Mungai wa jiji la Burlington, alipatikana na hatia ya kupokea mali ya wizi.

Kulinga na orodha hiyo, Antony Karia anayeishi jiji na Seattle, Washington atafurushwa kwa kuwa alihukumiwa kwa ulaghai, kutoa taarifa za uongo, na kutoroka baada ya kusababisha ajali, Boniface Mburu wa jiji la Marietta, Georgia aliyehukumiwa kwa kushambulia kwa kutumia silaha na kumiliki mali ya wizi.

Kevin Gunyanyi wa Lancaster aliyehukumiwa pia kwa kushambulia, kutoa vitisho, makosa ya kigaidi, na shambulio la kawaida na Collins Keanche wa Saint Cloud, Minnesotta aliyehukumiwa kwa kughushi hundi na ulanguzi wa fedha.

Utawala wa Trump pia umepanga kumfurusha mkenya aliyetambuliwa kama Isaac Githinji mkazi wa Apache Junction, Arizona ambaye analaumiwa kwa kutoroka kizuizini au kuepuka mashtaka, Moses Okoth wa jiji la Nashville, Tennessee kwa kushambulia mtu kwa kutumia silaha, Clement Mulovi wa Houston, Texas kwa ulaghai na Naserian Montet wa Spanish Fork, Uta asiyetakiwa Amerika kwa kushambulia na kukiuka amri ya mahakama.

Hatua hii imezua msisimko mkubwa miongoni mwa Wakenya waishio Amerika na familia nchini Kenya ambazo hutegemea misaada ya kifedha kutoka Amerika, kwani inaashiria utawala wa Trump unaendelea kukaza utekelezaji wa sheria za uhamiaji na ni hatari kubwa zaidi kwa jamii za wahamiaji kote nchini humo.

Kulingana na maafisa wa Wizara ya Usalama wa Ndani ya Amerika, hifadhidata ya serikali ambako orodha hiyo imeandaliwa itatoa kwa umma taarifa kuhusu maelfu ya kesi za uhamiaji, ikiwa ni hatua muhimu katika kutimiza ahadi za kampeni kuhusu udhibiti wa mpaka.

Waziri wa Usalama wa Ndani, Kristi Noem, anayesimamia mpango huo, alisema kuwa jukwaa hilo ni utekelezaji wa agizo la moja kwa moja kutoka kwa Rais Trump.

“Maafisa wa DHS wanatimiza ahadi ya Rais Trump na kutekeleza shughuli za kufurusha kwa wingi wahamiaji haramu, tukianza na wabaya kuliko wote,” alisema.

Jukwaa hilo linawalenga raia wa mataifa ya kigeni waliopatikana na hatia ya makosa makubwa ya jinai, kwa lengo la kuhalalisha kasi ya msako wa sasa.

Hifadhidata hiyo inaorodhesha wahalifu wanaohusishwa na magenge, uhalifu uliopangwa, ulanguzi na uuzaji wa dawa za kulevya, pamoja na hukumu za uhalifu wa kutumia nguvu na uhalifu wa kingono, ikiwemo makosa dhidi ya watoto.

Tovuti hiyo ina maelezo la jina la mhusika, picha yake, nchi ya asili, na mashtaka au hukumu walizopata kutoka kwa maafisa nchini Amerika.