Wakenya mabwanyenye wameficha Sh15 trilioni ughaibuni – Ripoti
BRIAN NGUGI NA PETER MBBURU
BAADHI ya Wakenya mabwanyenye wameficha zaidi ya Sh14.8 trilioni ambazo walizipata kwa njia zisizofaa katika akaunti za benki nje ya nchi, ripoti mpya imesema.
Ripoti hiyo ya shirika la Kimarekani imeonyesha kuwa watu hao ambao ndio baadhi ya matajiri wakubwa zaidi Kenya wamefanya hivyo kwa kuwa pesa hizo zilipatikana kwa njia haramu, hawataki kulipa ushuru ama kufuata sheria za fedha za Kenya.
Ripoti hiyo iliorodhesha Kenya, Yorodani, Urusi, Taiwan, UAE, Venezuela na Zimbabwe miongoni mwa mataifa ambayo yako na utajiri mwingi nje ya mipaka yake, ikilinganishwa na pesa ambazo serikali zake zinapata.
Kiwango hicho cha pesa zinazohifadhiwa na Wakenya ambazo haziwezikukaguliwa sasa kimebainika kuwa karibu mara tano ya bajeti ya Kenya ya 2018-19 ya Sh3 trilioni.
Ripoti hiyo ya shirika la NBER vilevile imesema kuwa Wakenya wanaohifhadhi pesa hizo hawajakiri ili zirejeshwe nchini ambako zinaweza kukaguliwa kubainika namna walivyozipata.
Hii ni licha ya waziri wa fedha Henry Rotich wakati wa kusoma bajeti ya mwaka wa fedha 2017-18 kuwapa Wakenya wenye mali mataifa ya nje mwaka mmoja kuirejesha nchini hadi Juni 2018.
“Kiwango cha utajiri uliohifadhiwa mataifa ya nje kinaibua mvuto, kwanza kinatoa picha ya tabia ya mataifa ya Africa na hapa inaonekana Kenya inaongoza,” akasema mchanganuzi kutoka Jijini Nairobi Aly Khan Satchu.
“Kuhifadhiwa kwa pesa hizo nje ya nchi ulikuwa mpango wa kuzitafutia mahali salama na wengi ni waliokuwa vigogo wa kisiasa. Lakini sasa kutokana na sheria mpya katika huduma za benki ambapo taasisi zinatakiwa kujua wateja wao, itakuwa vigumu kwao kuzitoa na zitashikwa,” akasema.
Mnamo 2016, nakala 11,500 za kibinafsi kutoka kwa kampuni ya sheria kutoka Panama, Mossack Fonseca, ambazo zilipatikana kimakosa zilionyesha namna Wakenya mabwenyenye hutumia akaunti za nje ya nchi kuficha utajiri wao uliopatikana kwa njia haramu.
Nakala hizo zilitaja watu 191 na kampuni 25 za nje ya nchi kuwa zilikuwa zikiwahifadhia mali yao.
Watu hao walitumia kampuni ghushi zilizoundwa kwa ajili tu ya kufanya biashara hizo za kuondoa pesa nchini, ili kuwakinga wasifahamike.
Ripoti za hivi majuzi zimeonyesha kuwa kiwango cha pesa ambazo Wakenya matajiri wamehifadhi katika benki za Uswizi kiliongezeka kwa asilimia 4.3 hadi Sh96 bilioni mnamo 2017 kutoka Sh92bilioni 2016.