Wakenya wafurika Tanzania kununua vitunguu baada ya zao kuadimika nchini
BEI ya vitunguu masokoni huenda ikaongezeka maradufu kufuatia uhaba mkubwa wa bidhaa hiyo, hali inayowalazimu wafanyabiashara wengi kusafiri hadi nchini Tanzania kuinunua.
Kutokana na uhaba huo katika maeneo yanayojulikana kwa uzalishaji mkubwa, bei ya vitunguu, hasa vile vinavyotumika sana, imepanda kwa kasi katika masoko mengi.
Katika Kaunti ya Kajiado, hasa maeneo ya Loitoktok ambako vitunguu hulimwa kwa wingi, wakulima wengi hawakupanda zao hilo msimu huu kutokana na gharama ya juu ya mbegu pamoja na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Katika eneo la Kimana, viungani mwa mji wa Loitoktok, mkulima Peter Mburu anasema kuwa gharama ya kilimo cha vitunguu imekuwa ya juu mno ikilinganishwa na mapato ya chini na ukosefu wa bei nzuri sokoni.
“Katika msimu huu, upanzi wa vitunguu ulikuwa wa chini sana, na hata mazao yalikuwa madogo. Hali hii imeathiri usambazaji wa vitunguu kwa wingi. Kwa sasa, bei ya mbegu ya kitunguu imefikia kati ya Sh36,000 hadi Sh40,000 kwa kila pakiti,” akasema Bw Mburu.
Aliongeza kuwa mabroka hununua vitunguu vilivyokauka kutoka kwa wakulima kwa bei ya juu ya Sh90 kwa kilo, hasa wakati ambapo hitaji ni kubwa na usambazaji umepungua.
Isitoshe, baadhi ya wakulima walipata hasara msimu uliopita baada ya kununua mbegu feki, jambo lililosababisha wengi wao kuhamia kilimo cha nyanya msimu huu.
Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo siku ya Jumatatu katika miji mikubwa ya Kaunti ya Kajiado ikiwemo Ngong, Ong’ata Rongai, Kiserian na Kitengela, ulibaini kuwa kilo moja ya vitunguu huuzwa kwa kati ya Sh130 hadi Sh150 kulingana na ukubwa wake.
Hii ni tofauti kubwa ikilinganishwa na miezi miwili iliyopita ambapo bei ya kilo moja ya vitunguu ilikuwa kati ya Sh60 na Sh80