Wakili Gicheru: Sikushurutishwa wala kutishiwa ili nijisalimishe ICC
Na VALENTINE OBARA
WAKILI Paul Gicheru anayedaiwa kushawishi mashahidi wajiondoe katika kesi iliyomkumba Naibu Rais William Ruto katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), ameambia mahakama hiyo hakushurutishwa na yeyote kujisalimisha.
Bw Gicheru ambaye alijisalimisha kwa ICC Jumatatu, amesema aliamua mwenyewe kujisalimisha.
“Nilijisalimisha kwa hiari Novemba 2, 2020. Sikushinikizwa na yeyote nijisalimishe. Nilijitolea mwenyewe na kwa gharama yangu binafsi. Hapakuwa na vitisho wala shinikizo,” akasisitiza.
Alikuwa akizungumza alipofika kizimbani kwa mara ya kwanza leo Ijumaa, ambapo ilikuwa ni kikao cha kupanga ratiba ya kusikizwa kwa kesi yake.
Ijapokuwa hakuhitajika kukiri wala kukanusha mashtaka katika kikao hicho cha kwanza, alikana kuhusika katika njama za kuhonga mashahidi waliokuwa wakitegemewa na upande wa mashtaka kwa kesi ya Dkt Ruto na mwanahabari Joshua arap Sang.
Kwa kawaida kikao cha kwanza huwa ni cha kumfahamisha kuhusu haki zake na masuala mengine yanayohusu uendeshaji kesi katika ICC.
Katika mashtaka yaliyosomwa, upande wa mashtaka ambao uliwakilishwa na Bw Anton Steynberg ulidai Bw Gicheru alihusika katika kuhonga mashahidi kati ya Sh1 milioni hadi Sh5 milioni, huku wengine wakiahidiwa kupewa ajira endapo wangeondoa ushahidi wao kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007.
Kwa jumla, kiwango kilichotajwa mahakamani kuwa kilinuiwa kutolewa kama hongo ni zaidi ya Sh10 milioni.
“Sina nia ya kukiri mashtaka kwa hivyo nataka kusema wazi na ieleweke kuwa madai dhidi yangu si kweli. Ni uongo. Yote sita ni uongo,” akasema.
Bw Gicheru ataendelea kukaa kizuizini ICC kwa muda, lakini yuko huru kuwasilisha ombi aachiliwe huru wakati kesi itakapokuwa ikiendelea.
Alistahili kushtakiwa pamoja na Bw Philip Kipkoech Bett, ambaye Kiongozi wa Mashtaka Fatou Bensouda aliomba mapema wiki hii serikali ya Kenya isaidie kumkamata na kumwasilisha kwa ICC.