Wakora wateka serikali
NA BENSON MATHEKA
WIZI wa pesa za kukabiliana na janga Covid-19 umetajwa kuwa kazi ya makundi ya uhalifu ndani ya serikali yanayoshirikiana na wafanyibiashara walaghai.
Kulingana na wanaharakati na wataalamu wa uchumi, Kenya itaendelea kupoteza mabilioni ya pesa za umma kwa miaka mingi kutokana na makundi haya ambayo wanasema yana nguvu hata za kuamua wanaochaguliwa kwenye vyeo vya kisiasa pamoja na usimamizi wa idara za serikali, mashirika na utawala wa kaunti.
“Makundi haya yalianza Kenya iliponyakua uhuru mnamo 1963, yanarithiwa na yanaendelea kuongezeka na kupata nguvu,” asema mwanaharakati Deborah Akumu.
Makundi haya yanahusika na maovu ya kila aina na hayawezi kuchukuliwa hatua kwa sababu yako na washirika wao katika idara ya polisi, mahakama, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na tume zinazopaswa kupigana na ufisadi.
“Idara hizi ni za kutakasa maovu yao. Hii ndio sababu wanaoiba pesa za umma na wanaochochea chuki za kikabila wanaepuka adhabu licha ya kujulikana wazi,” asema Bi Akumu.
“Wako na wanachama katika kila idara zote za serikali ikiwemo polisi, bunge na mahakama. Wako na washirika wao pia katika tume zinazopaswa kutetea mwananchi na hii imezifanya ziwe mihuri tu ya kuidhinisha malengo yao,” asema mwanaharakati mwingine aliyeomba tubane jina lake.
Kulingana na aliyekuwa Jaji Mkuu Dkt Willy Mutunga, makundi hayo yamefanya raia kuwa watumwa na yeyote anayejaribu kuyapinga hutishwa ama hata kuuawa.
Alisema wakuu wa makundi haya ni wanasiasa ngazi za juu na wafanyabiashara mabilionea wanaotumia kila mbinu kulinda maslahi yao kwa kukadamiza raia.
“Yanathibiti kila sekta ya uchumi, wanaendeleza ufisadi na ndio wanaoamua wanaoingia mamlakani,” alisema Dkt Mutunga mnamo 2016 siku chache kabla ya kustaafu.
Bi Akumu anasema ni makundi hayo yaliyonyakua na yanaendelea kunyakua ardhi za umma na kuendeleza ufisadi: “Kwa mfano, ni makundi hayo yaliyonyakua ardhi ya misitu ya Karura, Ngong na Mau. Sasa yamevamia ardhi ya soko la Gikomba ambayo inatumiwa na maskini kuuza mitumba. Ukitaka kujua ushawishi wao, walionyakua Msitu wa Ngong hawajaguswa walivyofanyiwa maskini Kariobangi, Ruai na kwingine.”
Kulingana na Bi Akumu, wanachama wa makundi haya ndio wamefanya maisha ya Wakenya kuwa magumu kwa kushawishi maamuzi muhimu serikalini.
Waziwazi
Makundi haya yameeneza mizizi yenye nguvu serikalini na biashara hivi kwamba wahusika wanaendeleza maovu yao bila kuficha na kujipiga kifua kwani wanajua hawawezi kupelekwa popote.
“Wanachama wa mitandao hii ya uhalifu hawatambui wala kuthamini utawala wa sheria kutokana na ushawishi mkubwa walio nao katika maamuzi yanayofanywa na serikali, lengo likiwa ni kulinda maslahi yao,” asema Bi Akumu.
Kulingana na Dkt Simon Kimotho, mtaalamu wa sera za kiuchumi, ni makundi haya yanayofanya bei za bidhaa muhimu na huduma kuwa ghali.
“Nchi hii imetekwa na majangili wa uchumi ambao wako na ushawishi na mizizi katika kila idara. Ndio wanaamua anayepatiwa tenda serikalini ili wapate kiinua mgongo. Ndio wanathibiti masoko na kuamua bei. Ni watu hatari kwa sababu ukijaribu kuwakosoa watakumaliza,” asema Dkt Kimotho.
Anasema hawa ndio wanaoingiza bidhaa kutoka nje ya nchi na kuzima juhudi zote za kufufua sekta muhimu nchini kama kilimo na viwanda.
“Wameporomosha sekta za kilimo kwa kuingiza mahindi na sukari nchini kutoka ng’ambo, wanavuruga mpango wa kufufua na kulainisha usimamizi wa mazao muhimu kama kahawa, chai na sukari ili waendelee kujitajirisha,” asema Dkt Kimotho.
Wanaharakati wanasema makundi haya yamepenya hadi makanisani na misikitini ili kuhakikisha mahubiri yanafuata mwelekeo unaowafaa.
Wataalamu wanasema makundi haya pia yanawalipa wataalamu na wasomi wasio na nia njema kubuni sera zitakazofanikisha ajenda zao.
Kulingana na Dkt Kimotho, vyama vikuu vya kisiasa ni mrengo wa kisiasa wa makundi haya kwa lengo la kutimiza mashahi yao: “Vyama vikuu vya kisiasa ni makundi ya Mafia yanayolenga kutimiza maslahi ya watu binafsi hasa viongozi wao. Havitilii maanani maslahi ya mwananchi kamwe.”
Sekta ya matatu pia imethibitiwa na makundi haya ya majangili wanaolindwa na wenye ushawishi katika taasisi za serikali na polisi.