Walimu Mombasa wahimizwa waondoe hofu wapimwe corona
Na WINNIE ATIENO
WALIMU Kaunti ya Mombasa wanahofia kwenda kupimwa virusi vya corona baada ya mwenzao kuaga dunia kutokana na ugonjwa huo ambao unaendelea kusambaa kwa haraka.
Wiki iliyopita mwalimu wa kiume alifariki katika hospitali ya kuu ya Pwani alikolazwa kwa kipindi cha wiki mbili baada ya kupatikana na virusi hivyo.
Shule za upili za umma ikiwemo Star of the Sea, Tononoka na Kashani zilifungwa baada ya walimu, wanafunzi na wafanyakazi wa shule hizo wapatao 28 kupatikana na virusi hivyo.
Taasisi hizo za elimu zilifungwa ili kuzuia kusambaa kwa maambukizi ya maradhi ya Covid-19 na vile vile kunyunyuziwa dawa maalum.
Wahudumu wa afya sasa wanaendelea kusihi vyama vya walimu kuingilia kati kuwashurutisha wlaimu kupimwa ili waweza kupokea matibabu na kupunguza maambukizi.
Wiki iliyopita walimu wakuu walikutana kujadili kuhusu janga hilo ambalo linaendelea kuzua taharuki Mombasa.
“Tulifuatilia baadhi ya watu wanaoshukiwa kuambukizwa na tukachukua sampuli na kupeleka kwa maabara ambapo iligunduliwa shule hizo tatu za upili, wengi waliathirika,” alisema afisa wa afya ya umma Pauline Oginga.
Bi Oginga alisema walipogundua wanafunzi, walimu na wafanyakazi 28 katika shule hizo waliathirika na ugonjwa huo walifanya vikao na vyama vya walimu na wadau wengine ili kuwahimiza wenzao kupimwa na kujua hali zao.
“Hii ni kwa sababu tumekuwa na wakati mgumu kuwahimiza walimu hao kupimwa ikizingatiwa kwamba huwezi kumlazimu mtu apimwe. Lakini tulifanya vikao na wawekezaji wa elimu na kuwaeleza umuhimu wa kuwapima walimu na pia tulisikiza upande wao ,” alieleza.
Bi Oginga, alisema idara yake itaendelea kulinada umma dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona, hata hivyo wakazi wlaitakiwa kuendelea kudumisha usafi kw akuosha mikono mara kwa mara, kuvaa barakoa na kutotangamana na watu.
“Tutaendelea kuwalinda walimu, wanafunzi na wafanyikazi katika shule. Tulichukua sampuli kutoka shule za upili za Star of the Sea, Tononoka na Kashani hapo dnipo tulipata visa vingi vya virusi hivyo,” akaongeza.
Mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir amekutana na walimu wakuu wa shule za upili zilizoko Mombasa ambapo wameelezea baadhi ya changamoto zao kipindi hiki cha janga la Covid-19.