Habari

Walimu wakuu wadai malimbikizo ya karo

October 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na FAITH NYAMAI

WALIMU wakuu wa shule za umma wanataka Wizara ya Elimu ielekeze wazazi kulipa karo ya shule kwa watoto wao ambao walirejea shuleni wiki iliyopita, wakisema wanafunzi wengi hawakulipiwa muhula wa pili.

Wakuu wa shule za upili ambao walizungumza na Taifa Leo walisema Ijumaa kwamba shule nyingi haziwezi kumudu gharama ya kuwaweka wanafunzi shuleni, kutokana na changamoto za kifedha.

Mwenyekiti wa Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari Nchini (Kessha), Bw Kahi Indimuli, alisema, shule nyingi zinategemea fedha kutoka kwa karo zinazolipwa na wanafunzi.

“Wakuu wa shule wanakabiliwa na wakati mgumu. Bila fedha, ni vigumu kuwalisha wanafunzi na pia kutimiza mahitaji yao ya bweni,” alisema Bw Indimuli.

Wiki iliyopita, Waziri wa Elimu, Prof George Magoha aliwaamuru wakuu wa shule wawaruhusu wanafunzi kurudi shuleni bila kulipa karo.

Prof Magoha aliwaomba wakuu hao wahakikishe kwamba hakuna mwanafunzi atafukuziwa karo, iwe ni shule za kibinafsi au za umma.

Hata hivyo, wakuu wa shule wanasema wazazi wametumia mwongozo wa waziri huyo na kuwapeleka watoto wao shuleni bila karo yoyote.

“Wazazi lazima watimize wajibu wao na kuwalipia watoto wao karo ya shule ya muhula wa pili. Wazazi walio na watoto katika shule za bweni wanajua kwamba wanahitajika kulipa ada za bweni. Wale wa shule za kutwa, huwa wanalipia tu chakula chao cha mchana,” akasema.

Wanafunzi wengi walikuwa hawajamaliza kulipa karo za muhula wa kwanza kabla ya shule kufungwa mnamo Machi, na kusababisha shule nyingi kujilimbikizia madeni makubwa zinayodaiwa na waliowasambazia bidhaa.

Bw Indimuli alisema pesa zilizotumwa na serikali wiki moja iliyopita zilikuwa chache sana, na hazitoshi kuendesha shule.

Muhula huu, wizara ilitoa jumla ya Sh14.4 bilioni kwa shule za msingi na sekondari kuwasaidia kujiandaa kwa ufunguzi wa pole pole.