Walimu wataka mara hii mwenzao ateuliwe mkuu wa TSC
SIASA za kumsaka mrithi wa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Kuajiri wa Walimu nchini (TSC) Nancy Macharia zimeanza kupamba moto baada ya walimu kushawishi kuteuliwa kwa mmoja wao.
Chama cha Walimu Nchini (KNUT) kimewataka makamishina wa TSC kuteua mwalimu aliyefuzu kwenye nafasi hiyo.
Knut imesema wanataka makamishna hao kuteua mkurugenzi mkuu wa TSC mapema huku Bi Macharia akitarajiwa kuanza likizo ya kustaafu wakati wowote.
Bi Macharia amesalia na miezi miwili kabla ya kustaafu baada ya kuhudumu kama mkurugenzi kwa mwongo mmoja.
“Tunaitaka serikali iajiri mkurugenzi mkuu wa TSC mapema, hatutaki nafasi hiyo ipeanwe kama kaimu na pia hatutaki mwanasiasa apewe nafasi hiyo.
Tunataka mwalimu, aliyesomea taaluma hii kutoka chekechea hadi kuwa hata Profesa,” alisema Dkt Malel Langat ambaye ni naibu mwenyekiti wa kitaifa wa Knut.
Akiongea kwenye mahojiano na Taifa Leo Mombasa, Dkt Langat alisema nafasi hiyo ikipeanwa kwa mwanasiasa walimu wataumia kwa kukosa kupiganiwa haki yao.
“Licha ya changamoto teli, Bi Macharia alijaribu kuweka msingi bora kwenye taaluma ya ualimu. Tunasubiri kwa hamu kuona mkurugenzi atakayeteuliwa, tunataka mtu ambaye atafanyia kazi na walimu na pia kuweka maslahi yetu mbele kisha kutulinda,” akaongeza Dkt Langat.
Alisema, Knut inataka mtaalamu ateuliwe TSC kwa sababu ataelewa changamoto za walimu kutoka chekechea na kutoa suluhu.
Vilevile alisema Knut inatumai Bi Macharia atatia saini makubaliano mapya (CBA) na walimu hao kabla ya kustaafu.
Kwenye makubaliano hayo, Knut imetoa pendekeza kwa kuongezwa kwa marupurupu ya walimu wanaofunza masomo ya sayansi kwa asilimia 10 kutokana na hatari ya kutumia kemikali kwenye maabara.
Mwezi uliopita, Bi Macharia aliwahutubia walimu wa shule za kitaifa na kuwaaga rasmi akisema amesalia na miezi miwili kabla aondoke mamlakani.
Alisema amepunguza mikutano ya hadhara akijitayarisha kuondoka mamlakani na kwenda nyumbani kulinda boma lake ambalo alisema alilitelekeza kufuatia ‘kazi’ ngumu.
“Nimekuwa nikifagia kona zote za boma langu hata kule ambako sikuwa nafikia sababu ya shughli za kikazi. Nimekuwa nikirauka kwenda kazini na kurudi nyumbani kuchelewa hata wikendi nimekuwa nikienda kazini na saa nyingine kupelekwa bungeni kujibu maswali,” alisema Bi Macharia.
Hata hivyo, alisema kazi hiyo si rahisi hasa migomo ya walimu inapotokea.
Bi Macharia alisema kwa miaka 30 amefanya kazi kwa tume hiyo baada ya kuajiriwa akiwa msichana mdogo na kupanda ngazi hadi kuwa mkurugenzi mkuu.