Habari

Walioachishwa kazi Choppies mjini Nakuru waelezea kero yao

September 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PHYLLIS MUSASIA

WAFANYAKAZI wa supamaketi ya Choppies mjini Nakuru wameelezea masikitiko yao kuhusu jinsi ambayo wamezidi kupokezwa barua za kufutwa kazi siku chache baada ya usimamizi wa dukakuu hilo kutangaza kuwa utafunga maduka 12 ya humu nchini.

Wale ambao tayari wametupwa nje wamesema kuwa wanasikitishwa na uamuzi huo ambao wanahisi haukuhusisha chama cha ushirika wa wafanyakazi wa kibiashara (KUCFW).

“Jinsi ambavyo tulipewa barua barua ilidhihirisha mambo mengi ambayo yamefichika. Tuliambiwa tukae nje hata kabla ya kulipwa pesa zetu,” akasema mmoja wa wale walioathirika.

Aliongeza kuwa wafanyikazi hao hawana imani ikiwa watalipwa mishahara yao kufikia Septemba 30 kama ilivyoandikwa kwenye barua hizo.

“Hatima yetu anayejua ni Mwenyezi Mungu pekee. Baadhi yetu ni wazazi wanaotegemewa na watoto wetu wako shuleni. Tuko pia na madeni ya benki mbalimbali na hatuji hali itakuwaje,” akasema mwathiriwa mwingine.

Alieleza kuwa aliripoti kazini kama kawaida Ijumaa wiki jana lakini alipotaka kurekodi kuwa alikuwa amefika, aligundua kuwa jina lake lilikuwa linakosekana kwenye listi.

“Nilishikwa na wasiwasi na nikataka kujua ikiwa jina langu lilisahaulika wakati wa kurodheshwa kwa majukumu ya siku. Meneja aliniita na kunieleza kuwa sikuhitajika kazini tena na hapo ndipo nilipokezwa barua yangu,” akaeleza.

Kabla ya Ijumaa mfanyakazi huyo alisema kuwa meneja wa duka hilo Bw Peter Wachira aliitisha mkutano wa wafanyikazi wote mnamo Alhamisi mwendo wa saa nane.

“Alitueleza kuwa alikuwa na ujumbe kutoka kwa wakurugenzi wakuu na ilikuwa vyema atueleze. Ilikuwa ni kupitia mkutano huo wa takribani muda wa saa moja hivi ndipo tulipata habari kuwa huenda tukapoteza kazi kutoka kwa mwajiri wetu,” akaeleza mfanyakazi mwingine aliyedai kukosa uhakika kuhusu muda ambao amebakisha kufanya kazi Choppies.

Ziara ya Taifa Leo kwenye duka hilo ilibaini rafu zisizokuwa na bidhaa huku duka nzima likionekana bila wanunuzi wengi.

Katika sehemu ya kulipia bidha, aliketi mwanadada mmoja aliyeonekana kukosa kazi kwa sababu hakukuwa na wateja wa kulipia bidhaa.

Baadhi ya wapishi walisema kuwa kazi imepungua kufuatia viwango vya chini vya chakula ambavyo vinaandaliwa kwa siku.

“Tulikuwa tukipika vyakula si haba. Wateja walikuwa wengi na hamna siku hata moja ambayo chakula kingebaki hapa. Wakati huu hali ni tofauti sana na baadhi yetu tumejawa na wasiwasi mwingi,” akasema mmoja wa wapishi.

Kufikia Jumamosi, wafanyakazi 18 walikuwa wamepokea barua zao huku wachache waliobaki wakionekana wenye wasiwasi mwingi.

Waathiriwa waliomba chama chao cha KUCFW kuingilia kati na kuhakikisha kuwa wanapata haki.

Juhudi za kumtaka meneja msaidizi Bw Peter Mukiri kuzungumza na Taifa Leo ziliambulia patupu kwani kila swali aliloulizwa alikosa kulitolea jibu.

Duka la Choppies limehudumu nchini kwa muda wa miaka minne tangu liliponunua baadhi ya bidhaa zake kutoka kwa duka lingine la Ukwala lililofifia.