Habari

Wanafunzi hawatapata vyeti baada ya KPSEA na KJSEA, asema waziri

Na MERCY SIMIYU October 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WANAFUNZI wanaofanya mitihani ya Kenya Primary School Education Assessment (KPSEA) na Kenya Junior School Education Assessment (KJSEA) hawatapatiwa vyeti mara baada ya kumaliza masomo yao ya shule ya msingi na shule ya sekondari msingi (JSS).

Badala yake, wanafunzi hao watapokea ripoti ya mpito mwishoni mwa Darasa la 6 ikieleza kwa undani utendaji wao, na nakala ya matokeo mwishoni mwa Darasa la 9, ambayo pia itakuwa ya maelezo badala ya alama kama A, B, C au D.

Taarifa hizo zitatumwa tu kwa Wizara ya Elimu kwa madhumuni ya kupanga nafasi za wanafunzi katika shule za Sekondari Pevu.

Hatua hii ni sehemu ya mabadiliko makubwa kutoka mfumo wa 8-4-4 hadi mfumo wa elimu unaoangazia umilisi (CBE).

Cheti cha elimu kitatolewa tu mwishoni mwa elimu ya msingi yaani baada ya Gredi 12 kabla ya mwanafunzi kujiunga na elimu ya juu au vyuo.

Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu, hatua hii inalenga kupunguza mashindano na mtazamo wa kushindwa miongoni mwa wanafunzi wadogo.

“Kutoa vyeti katika kiwango cha shule ya msingi chini ya 8-4-4 kulisababisha ushindani mkubwa na kuwakatisha tamaa watoto waliotazamwa kama walio ‘feli’. Kutokuwepo kwa vyeti mapema kutasaidia kuongeza motisha kwa wanafunzi kwa kuwa ripoti za KNEC zitaonyesha maendeleo yao kwa undani,” alisema Waziri wa Elimu, Bw Julius Ogamba.

Aliongeza kuwa badala ya vyeti, wanafunzi watapokea ripoti za tathmini zitakazoonyesha kiwango chao cha utendaji katika maeneo mbalimbali ya ujuzi.

“Kwa mfano, mwanafunzi anaweza kuwa hafanyi vizuri katika Hisabati lakini anafanya vizuri zaidi katika Kiingereza au Sanaa. Hii inawezesha kutambua nguvu zao na kuzikuza kadri wanavyoendelea,” alisema Bw Ogamba.

Kulingana na Baraza la Mitihani la Kitaifa la Kenya (KNEC), jumla ya wanafunzi 3,424,836 wanatarajiwa kufanya mitihani ya kitaifa mwaka huu. Kati yao, 996,078 watafanya KCSE, 1,130,669 watafanya KJSEA, huku 1,298,089 wakifanya KPSEA.

Bw Ogamba alisema kuwa mwishoni mwa Gredi la 12, wanafunzi watapatiwa Cheti cha Elimu ya Msingi (Kenya Certificate of Basic Education – KCBE), ambacho kitaonyesha umahiri wao katika ujuzi na maandalizi ya kujiunga na elimu ya juu.

“Vyeti baada ya shule ya Sekondari Pevi vitatolewa kulingana na mkondo wa masomo wa mwanafunzi — iwe ni katika sayansi, masomo ya kijamii au sanaa na michezo. Mfumo huu unarahisisha zaidi mpito kuelekea vyuo vikuu na taasisi za juu za mafunzo,” alifafanua.